KINGAZI BLOG: 11/09/16

HABARI KARIBU YAKO ZAIDI.

Breaking News
Loading...

Wednesday 9 November 2016

TANZIA:Yule Mtoto Aliyepandikizwa Betri kwenye Moyo Afariki Dunia

Mtoto Happiness Josephat (6) aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza betri moyoni katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), amefariki dunia.

Mama mzazi wa Happiness, Elitruda Malley amesema Happiness alifariki dunia ghafla juzi mchana.

Alisema   Jumapili, mtoto huyo alikuwa mzima na walikwenda kanisani kutoa sadaka ya shukrani kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa mambo aliyowatendea na wakarudi nyumbani salama.

“Jana tumeamka vizuri lakini ghafla hali yake ilibadilika akaanza kulalamika kuwa anajisikia vibaya, tukamkimbizia Hospitali ya Selian hapa Arusha lakini tukiwa njiani alifariki dunia,” alisema.

Elitruda alisema kifo cha mwanawe kimemhuzunisha mno na  daima atamkumbuka.

“Alikuwa tayari amesharudi shuleni, alikuwa akiniambia kuwa atasoma kwa bidii ili ndoto yake ya kuwa daktari bingwa itimie aweze kusaidia watu wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali,” alisema.

Hata hivyo, alisema maziko ya Happiness yanatarajiwa kufanyika leo huko Mbulu mkoani Manyara.

Mkurugenzi wa JKCI, ambako Happiness alifanyiwa upasuaji, Profesa Mohamed Janabi amesema taarifa hiyo imemshtua ikizingatiwa mtoto huyo alikuwa anaendelea vizuri.

“Sikuwa na taarifa, nitawasiliana na mama yake   tujue hasa shida gani ilitokea, maana zipo sababu nyingi labda alipita jirani na mitambo ya umeme au simu, hizo ni sehemu hatarishi kwa mtu aliyewekewa betri kwenye moyo,” alisema.

Happiness alifanyiwa upasuaji huo wa historia nchini Julai 15, mwaka huu katika Taasisi ya JKCI wa kuwekewa betri maalumu kwenye moyo ambayo kitaalamu inaitwa ‘pacemaker’.

Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibia mtoto huyo, wakati alipopekekwa hospitalini hapo, mapigo yake ya moyo yalikuwa 20.

Walisema  hali hiyo kwa mtoto si ya kawaida kwa vile  anapaswa kuwa na wastani wa mapigo 60 hadi 100 kwa umri wake.

Mtoto Happiness alizaliwa na tatizo hilo ambalo mara nyingi hali hiyo huwakumba watu wazima.

Moja ya ndoto za mtoto huyo ambayo alinukuliwa akiisema ni kuwa daktari bingwa wa kutibu magonjwa mbalimbali.

Tahliso yataja makosa ya waombaji wa mikopo

Jumuiya ya wanafunzi taasisi ya Elimu ya Juu,(Tahliso), imesema imebaini kuwa baadhi ya wanafunzi hawakuwasilisha vyeti vinavyohakiki hali zao ikiwamo vyeti vya vifo vya wazazi huku baadhi wakishindwa kuvithibitisha kwa kamishna wa viapo.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Tahliso, Stanslaus Kadugaliza katika taarifa ya Jumuiya hiyo iliyotolewa baada ya kufanyIka kwa kikao cha dharura kilichoshirikisha Wizara ya Elimu na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu wiki iliyopita.

Kadugalize amesema walibaini makosa hayo baada ya kuwataka wanafunzi hao waliokosa mikopo kuwasilisha majina yao.

Amesema kasoro nyingine zilizofanywa na wanafunzi hao ni kutumia namba ya mtihani tofauti na ile aliyoitumia katika udahili wa chuo Tume ya Vyuo Vikuu nchini.

Taarifa hiyo ya Tahliso iliwataka wanafunzi hao kukata rufaa  sasa kwa sababu dirisha lipo wazi na ni bure.

Obama ampongeza Trump, amwalika White House

 Rais Obama amempigia simu Donald Trump kumpongeza kwa ushindi uchaguzi wa urais ambapo pia amemwalika ikulu ya White House mnamo Alhamisi wajadiliane kuhusu shughuli ya mpito.

Obama pia amempigia Hillary Clinton na kumpongeza kutokana na alivyofanya kampeni.

Rais Obama atatoa taarifa zaidi Jumatano kutoka White House kujadili matokeo ya uchaguzi na hatua ambazo tunaweza kuchukua kama taifa kuungana tena pamoja baada ya kipindi cha uchaguzi huu uliokuwa na ushindani mkali", katibu wa ikulu amesema kupitia taarifa.

Taarifa kamili hii hapa:



Matokeo Marekani 2016: Trump ndiye Rais mteule wa Marekani, amshinda CLINTON majimbo muhimu.

 Wagombea urais wawili wakuu wa urais Marekani Hillary Clinton na Donald Trump wanakaribiana sana katika matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa.

Clinton ameshinda Virginia naye Trump akashinda Ohio, Florida, na North Carolina.

Kwa sasa Trump ana kura 222 za wajumbe na Clinton 209. Mshindi anahitaji kura 270 za wajumbe.

Lakini mgombea wa Republican Bw Trump ameshinda majimbo mengi ya kusini mwa Marekani naye Bi Clinton akashinda majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa makadirio ya shirika la utangazaji la ABC News.

Chama cha Republican kinaonekana kuwa njiani kuhifadhi wingi wa wabunge katika Bunge la Wawakilishi.

 Donald Trump alipakia picha hii kwenye Twitter, yake, mgombea mwenza wake na jamaa na marafiki wakifuatilia matokeo New York.

Kama ilivyotarajiwa, Bw Trump ameshinda katika ngome za Republican katika majimbo ya Alabama, Kentucky, South Carolina, Nebraska, Indiana, West Virginia, Mississippi, Tennessee, Oklahoma na Texas, ABC News wanakadiria.

Bw Trump pia anakadiriwa kushinda Arkansas, Kansas, North Dakota, South Dakota, Montana na Wyoming.

Shirika hilo linakadiria Bi Clinton atashinda ngome za Democratic majimbo ya New York, New Jersey, Connecticut, Massachusetts, Maryland, Vermont, Delaware, Illinois, Rhode Island na District of Columbia.

Mshindi anahitaji kupata kura 270 kati ya jumla ya kura 538 za wajumbe ndipo atangazwe mshindi.

 Upigaji kura umemalizika katika majimbo 39 na matokeo kamili yalitarajiwa mwendo wa saa 23:00 EST (04:00 GMT Jumatano - Saa moja asubuhi Afrika Mashariki), upigaji kura utakaomalizika Pwani ya Magharibi.

Matukio mengine makuu:
Bodi ya Uchaguzi Carolina Kaskazini imekubali kuongeza muda wa kupiga kura maeneo manane wilaya ya Durham ambapo kuna milolongo mirefu ya wapiga kura.

Mgombea wa Republican aliyeshindwa kwenye mchujo Marco Rubio amehifadhi kiti chake cha useneta Florida

Thamani ya pesa za Mexico, peso, imeshuka sana baada ya Trump kuonekana akiongoza Florida
Mtu mmoja alifariki kwenye ufyatulianaji wa risasi karibu na kituo cha kupigia kura jimbo la Azusa, California. Watu watatu walijeruhiwa.

Bw Trump, tajiri kutoka Manhattan, na Bi Clinton, anayetaka kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani, walipiga kura mapema Jumanne katika jiji la New York.

Bw Trump alizomewa alipofika kupiga kura yake Manhattan, akiandamana na mkewe, Melania, na bintiye, Ivanka.

Wawili hao wamekuwa wakifuatilia matokeo kutoka jiji la New York.

Clinton amepakia picha hii, pamoja na ujumbe wa shukrani kwa watu wote, licha ya matokeo ya usiku wa leo

Bi Clinton atahutubia wafuasi Javits Centre, Manhattan naye Bw Trump atahutubu katika hoteli ya Hilton Midtown.

Maafisa wa polisi zaidi ya 5,000 wametumwa jijini New York kuimarisha usalama.

Utafiti wa maoni wa baada ya upigaji kura, uliofanywa na ABC News, unaonyesha wapiga kura 61% hawampendi Bw Trump nao 54% ndio hawampendi Bi Clinton.

Mapema Jumanne, Bw Trump kwa mara nyingine alikataa kusema iwapo atakubali matokeo.

"Tutaangalia tuone vile mambo yatakuwa," aliambia Fox News, huku akidai kwamba kumekuwa na kasoro hapa na pale kwenye uchaguzi.

"Ninataka kila kitu kiwe wazi."

Katika baadhi ya vituo, mitambo ya kupigia kura ilifeli na kwingine kukawa na milolongo mirefu, lakini yalionekana kuwa matatizo ya kawaida.

Bw Trump, aliyezua utata kuhusu kuaminika kwa shughuli ya uchaguzi kwa kudai kura "zitaibwa" mapema, pia amewasilisha kesi ya dharura Nevada.

Maafisa wa Republican wamemshtaki msajili wa wapiga kura wilaya ya Clark, wakidai jimbo hilo lilifungua vituo vya kupigia kura muda mrefu kuliko inavyofaa.

Lakini jaji ameitupilia mbali kesi hiyo.

Kando na kura za urais, Wamarekani wamekuwa pia wakipiga kura za Maseneta, wabunge wa Bunge la Wawakilishi na Magavana.

Viti vyote 435 Bunge la Wawakilishi vilikuwa vinashindaniwa, na ABC News wanakadiria kwamba bunge hilo litabaki chini ya udhibiti wa Republican.

Lakini theluthi moja ya viti Seneti, ambao Republican wamekuwa wanaongoza, pia vinashindaniwa, na Democratic wanatumai wanaweza kudhibiti bunge hilo.

Jumla ya Wamarekani 45 milioni, idadi kubwa zaidi kuliko awali, walijitokeza kupiga kura mapema.
Bw Trump na Bi Clinton wanapigania kumrithi Barack Obama wa Democratic.

Rais Obama haruhusiwi kuwania kikatiba baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka minne.
Rais mpya ataapishwa tarehe 20 Januari 2017.

Makonda kupandishwa kizimbani Kisutu leo

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo atapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujitetea dhidi ya kesi ya madai ya Sh200 milioni  iliyofunguliwa na waliokuwa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mgana Msindai na John Guninita.

Makonda anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Seneni Mponda atatoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Kwa upande wa Msindai na Guninita wao wanatetewa na mawakili kutoka kampuni ya Uwakili ya BM, Benjamin Mwakagamba na Ester Shedrack.

Katika kesi hiyo ya madai namba 68 ya mwaka 2015, Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Mwakagamba, walifungua kesi wakiiomba Mahakama hiyo ya Kisutu kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja wao kiasi cha Sh100 milioni.

Wanadai kiwango hicho cha fedha kutokana na maneno ya kuwadhalilisha yaliyotolewa na Makonda wakati akiwa  Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), alipoitisha mkutano na waandishi wa habari.

Walalamikaji hao pamoja na hayo, wanaiomba Mahakama hiyo itoe zuio  la kudumu kwa Makonda  asizungumze  tena maneno ya kashfa dhidi yao wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.

Pia, wanaomba Makonda kulipa riba na gharama za kesi.

Walidai kuwa Makonda  wakati akiwa katibu uhamasishaji chipukizi wa CCM,  katika mkutano wake alitoa maneno akidai kuwa Msindai na Guninita ni vibaraka wanaotumiwa kuharibu chama cha CCM kwa nguvu ya fedha.

Msindai na Guninita wanadai maneno hayo yaliyotolewa na Makonda  yamewadhalilisha kwa jamii na kuwafanya waonekane kuwa ni watu wasiofaa kuwa viongozi.

Source: Mwananchi

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Novemba 9



 

Gallery

Popular Posts

About Us