TUNAKULETEA MFULULIZO WA UIBUAJI WA UBADHILIFU MKUBWA WA FEDHA KATIKA MIRADI MBALI MBALI YA MAENDELEO KUTOKA KWA MKAGUZI NA MDHIBITI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI (CAG) | KINGAZI BLOG

HABARI KARIBU YAKO ZAIDI.

Breaking News
Loading...

Tuesday 18 April 2017

TUNAKULETEA MFULULIZO WA UIBUAJI WA UBADHILIFU MKUBWA WA FEDHA KATIKA MIRADI MBALI MBALI YA MAENDELEO KUTOKA KWA MKAGUZI NA MDHIBITI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI (CAG)

1..Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Aibua Ubadhirifu wa Kutisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

UBADHIRIFU wa kutisha unaohusisha mabilioni ya fedha, umefichuliwa kwenye Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ukihusisha uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni. 

Wanaodaiwa kuhusika na utafunaji wa mabilioni hayo, walitumia mabadiliko mapya ya usajili wa vitambulisho, yaliyoigharimu serikali kupitia manunuzi yasiyo na tija huku wadanganyifu wakitumia mianya iliyopo kujinufaisha wenyewe kinyume na taratibu. 

Kutokana na hali hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, aliagiza wale vote waliohusika na ubadhirifu na udanganyifu wa mabilioni ya fedha, wachukulie hatua kali. 

"Ukaguzi umejiridhisha kwamba, uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya taifa,"alisema.
 

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)    imeonesha ubadhirifu katika eneo la usajili na utambuzi ambako Sh bilioni 1.2 zililipwa kwa huduma za bima kupitia dalali wa Bima M/s Aste Insurance Brokers Company Limited. Kiasi hicho kililipwa zaidi ya gharama halisi isivyostahili.

Huduma hizi zilipaswa kugharimu Sh milioni 450.2, lakini mamlaka ililipa Sh bilioni 1.7. CAG alibaini kuwa dalali huyo wa bima, alitumia akaunti za biashara katika kupokelea fedha za malipo ya bima ya Sh bilioni 1.7 badala ya akaunti ya amana isivyostahili.

Kwa hali hiyo, CAG amependekeza kampuni ya uwakala wa bima irejeshe Sh bilioni 1.2 zilizolipwa zaidi isivyostahili; na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya Astery Ndege na kampuni hii kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kutoka mamlaka. 

Ubadhirifu mwingine alioutaja ulikuwa ni manunuzi ya bima ya vifaa vya usajili na magari yaliyotumika katika mradi wa vitambulisho vya Taifa ya jumla ya Sh milioni 494, yaliyofanyika bila kukihusisha Kitengo cha Manunuzi.

CAG pia ameshauri hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi waliohusika katika udanganyifu, uliobainishwa na kutozingatia sheria za manunuzi ya umma na kuisababishia Mamlaka gharama zisizo na tija sanjari na kuhakikisha kuwa wahusika wanafidia hasara iliyopatikana, kisha kuhakikisha udhibiti wa vifaa. 

Uhakiki wa leja za mafuta, pia ulibaini kuwa lita 1,110 za mafuta ya dizeli yenye thamani Sh milioni 2.2 zilitumika kwa shughuli zisizo za Mamlaka.

Pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilikopa Sh milioni 455.3 kutoka NIDA kwa ununuzi wa magari manne mwaka 2014, ambazo hadi ukaguzi unafanyika Oktoba 2016 fedha hizo hazikuwa zimerejeshwa. 

Uhakiki wa fomu zenye ‘Barcode’ zilizotengenezwa kupitia mpiga chapa binafsi M/s MFI Solution, ulibaini kuwa fomu 7,762,907 zenye thamani ya Sh bilioni 2.5 zilizopokelewa na mamlaka hazikutumika.

Kadhalika, ilibainika kuwa fomu 8,220,000 zenye thamani ya Sh milioni 519.6 zilizochapishwa tangu mwaka 2011/2012 hadi 2013/2014 hazikutumika; hivyo kutelekezwa katika stoo za TANITA. 

“Hali hii ilitokana na mamlaka kutokuwa na Mpangokazi, hivyo kuingia hasara ya Sh milioni 932.8,” ilisema ripoti hiyo.

Matengenezo ya magari 
Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 mpaka 2015/2016, Mamlaka ilifanya matengenezo ya magari kupitia gereji binafsi yaliyogharimu Sh bilioni 1.3. 

Nida pia ilifanya matengenezo yaliyogharimu Sh bilioni 1.1 yaliyofanyika na kulipwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi unaothibitisha kuwapo kwa ubovu wa gari na mahitaji ya matengenezo husika.

Pia kulikuwa na matengenezo yaliyogharimu Sh milioni 197.2, yaliyofanyika na kulipiwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi wa awali wala ukaguzi baada ya matengenezo.

 Ripoti imeeleza kuwa ukaguzi ulibaini malipo ya Sh milioni 42.7 yalifanyika zaidi ya madai stahili kutokana na udanganyifu wa kuongeza tarakimu katika hati za madai na kutumiwa kwa hati moja ya madai zaidi ya mara moja katika malipo ya kuanzia mwaka 2012/2013 hadi 2015/2016.

Ajira za muda na za kudumu 
NIDA imegundulika kuwa ilikiuka sheria katika ajira za muda na za kudumu, zilizofanywa na mamlaka kuanzia mwaka 2012 hadi 2015, ambapo vibarua 1,071 walipatikana kwa kupigiwa simu bila kutangaza mahali popote kinyume na Sera ya mamlaka hiyo. Ukaguzi ulibaini kuwa NIDA iliomba kupatiwa vibarua kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Chuo cha Utumishi wa Umma wapatao 415.

Lakini baada ya kupatiwa vibarua hao, mamlaka haikuwatumia na kubainisha kwamba wangetumiwa siku za baadaye. Ripoti ilifafanua kuwa mamlaka iliamua kuajiri vibarua wengine wapatao 882 bila kutangaza mahali popote, tofauti na watumishi 415 ambao walikwishapatiwa. Pia Septemba 2015 Mamlaka iliajiri watumishi 213 licha ya kibali cha kuajiri kutoka Utumishi kuisha tarehe Aprili 2015.

NIDA pia inatuhumiwa kufanya malipo Sh milioni 16.6 ya kiinua mgongo kwa vibarua, kinyume na mkataba wa ajira ya muda na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. 

Ubadhirifu mwingine uligundulika kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli, yaliyonunuliwa na mamlaka yenye thamani ya Sh bilioni 2.3, yaliyotolewa kwenye magari na majenereta, ambapo hayakuthibitika matumizi yake kutokana na sababu mbalimbali.

CAG pia amebaini upotevu wa vifaa vyenye Thamani ya Sh milioni 93.7 katika stoo ya mamlaka. Ukaguzi umebaini kuwa hakukuwa na taarifa rasmi kutoka kwa mtunza stoo juu ya upotevu huo, licha ya kufahamu kuhusu upotevu wa vifaa hivyo. Vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 991.4 havikutumika tangu kununuliwa kwake katika vipindi tofauti kuanzia Machi 2013 hadi Oktoba 2016.

Udanganyifu mwingine ulifanyika katika ushindanishi wa wazabuni katika ununuzi wa vifaa vya TEHAMA. Nida ilifanya manunuzi ya Ipad zenye thamani Sh milioni 63.4 zilizonunuliwa kutoka kwa M/s Elite computers baada ya kuonekana kukidhi vigezo vya ushindani na kupewa zabuni saba (7) tofauti. Lakini taarifa za wazabuni ambao waliainishwa kuwa washindani katika zabuni hii, M/s Prudent Enterprise na M/s Morex General Enterprise zilighushiwa; na wazabuni hawa hawakuhusishwa wala kutoa nukuu za bei.

Upangishaji nyumba Mamlaka ilitoa zabuni ya kuipangisha Ofisi ya Mamlaka kwa Mary Mwema kupitia barua ya maombi ya tarehe 06.05.2012 ambapo tangazo la zabuni husika ni la tarehe 25.05.2012 baada ya tarehe ya kuomba.

 “Zabuni husika haikupitia Kitengo cha Manunuzi na haikuwa imeidhinishwa na Bodi ya Zabuni,” inasema ripoti hiyo. 

Pia ripoti ilifafanua kuwa mzabuni wa upangishaji wa jengo la ofisi ya John Masenga haukujumuishwa kwenye mchakato wa tathmini ya kitaalamu licha ya kukidhi vigezo.

NYINGINE NI HII

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini kasoro katika mambo matano baada ya kufanya ukaguzi wa hesabu za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

Ripoti ya CAG imekuja wakati wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wakiwa wamesimamishwa kazi tangu Julai mwaka jana kupisha uchunguzi.
 
Ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni Aprili 13 mwaka huu, ikiwa ni siku chache tangu CAG, Profesa Mussa Assad aikabidhi kwa Rais John Magufuli.
 
Kasoro zilizobainika katika mfuko huo ni kiwango cha chini cha ukaliwaji wa majengo, usimamizi na udhibiti wa mikopo ya vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, udhaifu katika uwekezaji wa ardhi.
 
Ripoti hiyo inabainisha kasoro katika Shamba la Dungu na mradi wa uwekezaji Tuangoma na kasoro nyingine ni katika mkataba wa mshauri katika ununuaji wa Pan Africa Energy Limited kwa Sh551.61 milioni.
 
Ripoti inaonyesha kuwa NSSF imewekeza kwa kiasi kikubwa katika majengo ya kupangisha kwa wateja kama vile hoteli, kampuni, watu binafsi na kutumia sehemu nyingine ya majengo hayo kama ofisi zake.
 
Imegundulika kuwa, kiwango cha upangaji katika majengo tisa ya uwekezaji kilikuwa chini ya kusudio la kiwango cha soko cha asilimia 80. Ripoti inaonyesha kuwa kiwango cha upangaji kilikuwa kati ya asilimia 0 na 43.
 
Rasilimali hizo za uwekezaji katika majengo zinajumuisha hoteli ya Mwanza, Kigoma, jengo jipya la biashara la Old Moshi -Arusha, jengo jipya la biashara la Kaloleni (Arusha), jengo jipya (Kahama), Njiro (Arusha), jengo kubwa la kibiashara Kilimanjaro, Mafao House (Ilala) na jengo kubwa la kibiashara la Morogoro.
 
Mbali na hali hiyo CAG amebaini kuwa NSSF ilisimamisha kutoa mikopo kwa wanachama wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo Juni, 2016 ili kuimarisha usimamizi na kuhakikisha kuwa kuna ukusanyaji wa marejesho ya mikopo.
 
Hata hivyo, mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamisha utoaji, ilikuwa na mapungufu ikiwamo mikopo ya Sh1 bilioni iliyotolewa kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo zaidi ya kiwango cha ukomo.
 
Ripoti inaonyesha NSSF ilitoa Sh21.3 bilioni kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Bunge (National Assembly Saccos) na Sh2.2 bilioni kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Jumuiya ya Ndugumbi (Ndugumbi Community Saccos).
 
Utoaji huo wa mikopo ulizidi kiwango cha ukomo kwa Sh1 bilioni, lakini menejimenti ya NSSF ilieleza kwamba mikopo kwa wanachama wa Bunge ilitolewa kama mpango maalum wa kuvutia wanachama wapya kwenye mfuko.
 
Pia, kuna vyama vya ushirika vya akiba na mikopo vilivyopewa zaidi ya asilimia 50 ya mali zote ilizonazo.
 
Pia, CAG ameeleza kuwa ushuru wa stempu ulikuwa haujalipwa kwa vyama vinne vya ushirika ambavyo vilipewa mikopo.
 
Vyama hivyo ni Masoko Madogo Madogo ambacho hakijalipa Sh500 milioni, Ngima (Sh500 milioni), Mafanikio (Sh490 milioni) na Mount Meru (Sh260 milioni).
 
Udhaifu uliogundulika kwenye Uwekezaji wa Ardhi
Kwa mujibu wa CAG, taarifa za fedha za NSSF zilionyesha kuwa iliwekeza kwenye viwanja (Benki ya Ardhi) kwa thamani ya Sh97.2 bilioni, lakini imebainika kuwepo na mapungufu katika ununuaji na uwepo wa ardhi zilizonunuliwa.
 
Ripoti inaonyesha kulikuwa hakuna mipango na upembuzi yakinifu kuhalalisha sababu za kuwekeza katika rasilimali kinyume na aya ya 3.3 ya Sera ya Uwekezaji ya NSSF ya mwaka 2012 inayolitaka shirika hilo kuwekeza rasilimali zake katika miradi inayolipa zaidi ili kuweza kunufaisha wanachama wake.

“Sikuweza kupata hati ya umiliki ya viwanja/mashamba vinne kwa sababu vipo katika mzozo wa umiliki.  Viwanja hivi vilikuwa ni Nunge Beach kilichopo Bagamoyo chenye ukubwa ekari 67.35, kiwanja namba 146/4 Barabara ya Old Moshi kilichopo Halmashauri ya jiji Arusha, Clement Mabina Farm Bugando Magu na kiwanja namba 98 Barabara ya Nyerere (Pugu) Temeke chenye mita za mraba 8,825,” inaeleza ripoti ya CAG.
 
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mfuko uliingia mkataba na Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa ajili ya kununua viwanja 692 (viwanja 405 eneo la Kiseke na 287 Bugarika) kwa Sh1.89 bilioni.
 
Hata hivyo, ni viwanja 156 tu vilielekezwa Kiseke; wakati hakuna kilichoelekezwa upande wa Bugarika.
 
Pia, imesema kulikuwa na shamba namba 113 lililonunuliwa kwa Sh1.26 bilioni lililopo Mapinga, katika Manispaa ya Kinondoni lenye ukubwa wa hekta 127, lakini ni hekta 58 tu zilizokuwa zimetengwa na kufanyiwa kazi.
 
Ununuaji Pan Africa Energy
Dosari nyingine katika ripoti hiyo ni mkataba wa NSSF na Yakubu and Associates Chambers uliosainiwa Februari 12, 2016 kwa lengo la kutoa huduma ya ushauri ili kuwezesha kupatikana kwa mshirika Kampuni ya Pan Africa Energy Limited kwa ada ya utaalamu ya Sh551.61 milioni kwa ajili ya matumizi ya ziada na kodi za ndani.
 
Ripoti hiyo inaeleza mshauri huyo hakuwa na uzoefu uliohitajika kama ilivyoelekezwa kwenye hadidu za rejea iliyohitaji uzoefu wa mali zisizohamishika za ndani na mambo ya mazingira, ushauri wa kodi za ndani na nje na leseni na kanuni za mfumo wa hydrocarbon.
 
Pia, iligundulika kuwa Kampuni ya Yakubu and Associates Chamber ndiyo iliyokuwa imesajaliwa mwaka huohuo wa kukaribisha zabuni na hivyo washauri hawakuwa na uzoefu na mazingira ya ndani.
 
Mshauri alitakiwa kukagua taarifa ya uchunguzi iliyoandaliwa chini ya mkataba namba NSSF/CS/20/2014-2015 ulioingiwa Desemba 11, 2014 kwa ajili ya kutoa huduma ya ushauri katika ununuzi wa Kampuni ya Pan Africa Energy Limited. 
 
Kanuni iliyotumika ambayo ni namba 257(2)(a) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya mwaka 2013 (PPR, 2013), haikuwa sahihi.
 
Mkataba ulikuwa umeisha muda wake tangu Aprili 26, 2016, lakini uliongezwa muda kupitia kanuni namba 111(1) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya mwaka 2013 (PPR, 2013) inayomruhusu ofisa masuuli kuongeza muda wa mkataba na kuelezea sababu ya kufanya hivyo.
 
Ripoti ya CAG inasema mshauri aliwasilisha bili namba 01031604 ya Machi 1, 2016, lakini mpaka kufikia Oktoba 7, 2016 malipo yalikuwa hayajafanyika.
 
Kutokana na kasoro hizo, CAG ameeleza kuwa NSSF haikufuata vigezo vya kuchagua mshauri kama vilivyoainishwa kwenye Kanuni za Manunuzi ya Umma na Hadidu za Rejea (ToR) zilizoandaliwa na Bodi ya Wadhamini.
 
Pia, ameishauri menejimenti ya mfuko huo kuvunja au kusimamisha mkataba kwa kuwa mshauri hakuwa na uzoefu wa kutosha kufanya kazi hiyo.
 
Shamba la Dungu, Tuangoma 
Ripoti ya CAG inaeleza kuwa NSSF iliingia mikataba yenye thamani ya Sh165.4 bilioni kwa ajili ujenzi wa kijiji cha kisasa katika shamba la Dungu na Tuangoma Kigamboni katika Manispaa ya Temeke Dar es Salaam. Mfuko ulikuwa umeshaingia gharama ya Sh73.4 bilioni.
 
CAG anaeleza kuwa miradi ya mfuko huo ilitekelezwa bila kufanya upembuzi yakinifu ambao ungeipa menejimenti uhakika wa uwekezaji. Kwa sababu hiyo CAG ameshindwa kupata misingi na vigezo vilivyoshawishi maamuzi ya menejimenti kuwekeza, malengo ya uwekezaji na mipango ya kurudisha fedha zilizowekezwa.
 
Kutokana na hali hiyo, NSSF iligundua kuwa sehemu ya ardhi ya shamba la Dungu ilikuwa inamilikiwa na Shirika la Nyumba Taifa (NHC), hivyo baadhi ya ujenzi ulihamishiwa Tuangoma.
 
Hata hivyo, menejimenti haikuweza kutoa nyaraka za ununuzi wa viwanja vya Tuangoma na kama vilikuwa vina ukubwa sawa, vinauzika kwenye soko na kiwango cha kurudisha uwekezaji kama ilivyo kwa Dungu.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

    0 comments:

    POST A COMMENT

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us