SERIKALI nchini Swaziland imeziagiza shule zake kufundisha somo la dini ya Kikristo pekee, hatua iliokosolewa na wadau mbalimbali kwa kuwa haiheshimu dini nyengine.
Agizo hilo lilitolewa wiki iliyopita na Wizara ya Elimu nchini humo, ambapo ilipita shuleni ikiwaagiza walimu wakuu wote kuhakikisha mtaala hautaji dini nyingine zaidi ya Kikristo.
Sahid Matsebula, ambaye ni Muislamu anayefanya kazi msikitini karibu na Mji Mkuu wa Mbabane, alinukuliwa akisema kwamba sera hiyo huenda ikazua wasiwasi wa kidini katika ufalme huo.
''Serikali ina mpango gani kwa watoto wetu ambao si Wakristo? Ambao licha ya kujifunza wakiwa nyumbani, mambo mengine wanapaswa wajifunze wakiwa shuleni,” alisema.
Sera hiyo mpya imekuja baada ya raia kulalamika kuhusu wahamiaji wa Bara la Asia na wale wa Kiislamu kwamba wamekuwa wakiingia nchini humo hatua iliyolazimu Bunge kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo.
Wahamiaji wengine tayari wamerudishwa makwao na Waziri wa Biashara, Jabulani Mabuza ameliambia Bunge kwamba wameanza kutunga sheria itakayowazuia wahamiaji kuanzisha biashara nchini Swaziland.
Rais wa Baraza la Makanisa nchini humo, Stephen Masilela ameunga mkono mtaala huo mpya.
''Ukristo ndio msingi wa kujengwa kwa taifa hili,” alisema.
Hata hivyo, Taifa la Swaziland linaloongozwa na Mfalme Mswati wa tatu tangu mwaka 1986, lina idadi ndogo ya waumini wa Kiislamu.
Sera hiyo ya kufundisha dini ya Kikristo pekee shuleni, pia imekosolewa na mwandishi Nomsa Mbuli wa gazeti la Times of Swaziland.
“Kinachoinua dini moja juu ya nyengine ni nini wakati ambapo Katiba inaagiza usawa wa kidini?” alihoji.
0 comments:
POST A COMMENT