Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inapenda kuuarifu umma kuwa, uhakiki wa ubora wa wanafunzi wa elimu ya juu
hufanyika kwa mujibu wa Kifungu 5(1)(b)(c) cha Sheria ya
Vyuo Vikuu Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania.
Katika kutekeleza jukumu hili Tume ilianza zoezi la uhakiki kuanzia mwezi Agosti 2016. Hadi kufikia Februari 2017 zoezi
hilo lilikuwa limekamilika kwa vyuo 67 kati ya 84 vinavyotoa shahada ya kwanza.
Hii ni mara ya kwanza uhakiki wa sifa za wanafunzi wa vyuo vyote nchini kufanyika kwa wakati mmoja. Lengo la uhakiki lilikuwa kujiridhisha kuwa wanafunzi waliopo vyuoni ni wale waliodahiliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na kwamba wanakidhi vigezo stahiki.
Uhakiki ulifanyika kwa kulinganisha taarifa za TCU na zile zilizowasilishwa na vyuo. Uhakiki huo ulihusisha jumla ya wanafunzi 131,994 waliopo vyuoni kwa mwaka wa masomo 2016/17.
Baada ya kulinganisha orodha zilizowasilishwa na vyuo na ile ya TCU ilibainika kuwa wanafunzi 123,827 sawa na asilimia 93.8 wana sifa stahiki. Aidha jumla ya wanafunzi 8,167 sawa na asilimia 6.2 tu walibainika kuwa na kasoro katika taarifa za sifa zao.
Kufuatia hali hiyo, Tume ilitoa taarifa kwa umma kuwaomba wanafunzi kurekebisha dosari hizo kwa kuthibitisha taarifa zao kupitia vyuo husika ifikapo tarehe 28 Februari 2017 ili kuweka kumbukumbu sahihi za mwanafunzi.
Hata hivyo imebainika kuwa taarifa hiyo imepokelewa kwa mtazamo na hisia tofauti na hivyo kusababisha mkanganyiko vyuoni. Umma unaarifiwa kwamba haikuwa nia wala lengo la Tume kusababisha mkanganyiko huo.
Kwa kuwa uhakiki wa sifa za wanafunzi ni kazi endelevu ya Tume na kutokana na maombi ya wadau mbalimbali, Tume sasa itaendelea kuwasiliana moja kwa moja na vyuo katika kukamilisha zoezi hilo.
Hivyo wanafunzi wote waliokuwa wameorodheshwa katika taarifa iliyotolewa awali wanaombwa kuwa watulivu na kuendelea na masomo yao kama kawaida.
Aidha ifahamike kuwa wanafunzi waliokuwa wameorodheshwa siyo kwamba wamethibitika kuwa hawana sifa stahiki bali kuna dosari katika taarifa zao. Ndiyo sababu Tume iliwaomba kuthibitisha taarifa zao ili kuondoa dosari hizo.
Imetolewa na
Kaimu Katibu Mtendaji
24 Februari 2017