MWILI wa aliyekuwa Kiongozi wa Jumuiya ya Freemason Tanzania na Afrika Mashariki, Sir Jayantilal Keshavji Chande (89) ‘Andy’ Chande, umewasili juzi kutoka jijini Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa wafanyakazi wa Sir Chande ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kiongozi huyo aliyefariki juzi alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo.
“Mwili wake umeshawasili tangu jana (juzi) saa 2:30 usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) na wamerudi wote pamoja na familia yake yaani mkewe na watoto watatu waliokuwa wakimuuguza,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alisema kwa sasa mwili huo umehifadhiwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, ukisubiri maziko yatakayofanyika Jumanne ijayo.
Mbali na hilo pia alishangazwa na kusambaa kwa taarifa za kifo hicho kwa haraka juzi kwa kuwa familia hadi jana mchana ilikuwa haijapata taarifa rasmi.
“Mzee ni mtu mkubwa si Tanzania tu hata India, Marekani wote wameandika habari zake baada ya kusikia katika mitandao, lakini bado watu hawajaanza kuja kutoa pole, wengi wanapiga simu kuuliza tu kama ni kweli sisi tumeshangaa taarifa hizi mmezitoa wapi wakati hakukuwa na mtu aliyetoa habari kutoka katika familia jana,” alisema mfanyakazi huyo.
Alisema Sir Chande ambaye anatarajiwa kuchomwa Jumanne katika eneo la Makumbusho, aliugua tumbo kwa kipindi cha wiki moja wakati ugonjwa wake mkubwa uliokuwa ukimsumbua ulidaiwa kuwa ni shinikizo la damu.
Alisema vikao vya familia bado vinaendelea na kwamba wageni kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kuingia kuanzia Jumapili kuhudhuria mazishi hayo.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jioni na msemaji wa familia ya Sir Chande ambaye ni mtoto wake, maziko ya kiongozi huyo yatafanyika Jumanne saa nne asubuhi katika makaburi ya Makumbusho jijini Dar es Salaam.
“Taratibu za kuaga mwili wa Sir Chande zitafanya siku hiyo hiyo kuanzia saa 2.30 asubuhi nyumbani kwake,” ilieleza taarifa hiyo.
FAMILIA YAMWELEZEA
Katika taarifa, familia yake pia ilimwelezea Kiongozi huyo kama mtu aliyekuwa na hekima ambapo mara nyingi alikuwa anaisaidia Serikali na Watanzania na watu wengine duniani kote kwa kujihusisha na shughuli za kijamii, uchumi na misaada ya kibinadamu.
“Katika kutambua hilo, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza alimtunuku medali ya heshima ya kuwa Commander of the Civil Division of the Most Excellent Order of the British Empire (KBE),” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, wakati akitoa maoni ya tuzo hiyo alisema anashangilia kushuhudia Mtanzania aliyestahili kutunukiwa ‘Order of Knighthood in the British Empire’.
Familia yake pia imesema Chande aliwahi kupewa tuzo ya heshima ya Pravasi Bharatiya Samman kutoka kwa Rais wa India ambayo inatambulika kwa kiasi kikubwa nchini India kama mwanachama wa Diaspora.
Mwaka 2004, Chande alichapisha hotuba zake pamoja na mafundisho na habari kuhusu Freemason katika kitabu kinachoitwa Whither Directing Your Course na mwaka 2011 alichapisha kitabu kingine cha Transitions of a Life na kingine ‘A Knight in Africa: Journey From Bukene.
Vitabu vyake viligusa maeneo mbalimbali ikiwemo historia, biashara, mazingira, elimu na mambo ya kijamii.
Taarifa hiyo ya familia pia imeelezea namna Sir Chande alivyoshiriki katika harakati za ukombozi na uhuru nchini.
Inaelezwa uzalendo wa Sir Chande katika taifa kwa mara ya kwanza ulijitokeza mwaka 1967 katika harakati za maazimio ya Arusha wakati wa biashara ya familia yake, kiwanda cha Chande Industries Limited kilitaifishwa kwa Serikali Februari 7, 1967.
Hayati Mwalimu Nyerere alimwalika Chande kusaidia kuanzishwa kwa Shirikisho la viwanda vya kusaga na kuchakata (National Milling companies).
Alikubali kwa uaminifu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa National Milling Corporation kwa miaka mitano, baada ya kustaafu alitumikia kama mshauri wa Bodi ya Wakurugenzi.
Kati ya mwaka 1958 hadi 1961 kabla ya uhuru wa Tanzania, Sir Chande inaelezwa alitumikia katika nafasi ya mwanachama wa Legislative Council (LEGICO ).
Mwaka 1959, alipata nafasi ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Serikali ya Uingereza, Ian McLeod, kuhusiana na mapendekezo ya Uingereza kutoa uhuru wa kujitawala kwa Tanganyika.
Baada ya uhuru, Chande inaelezwa alishiriki katika shughuli mbalimbali nchini hasa za kijamii na kiuchumi.
Kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa Mwenyekiti au kama mwanachama wa Bodi ya Wakurugenzi wa makampuni kadhaa ya umma na binafsi ikiwa ni pamoja na Benki ya Barclays Tanzania na Uganda na pia mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na Shirika la Reli la Afrika Mashariki na East African Harbors Corporation.
Kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Sir Chande, aliteuliwa kuwa mwanzilishi na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na baadaye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Bandari Tanzania na wa Tanzania Railways Corporation.
Inaelezwa pia Chande alikuwa anajishughulisha na masuala ya kisiasa na kidiplomasia, wakati mmoja aliwahi kuwa mshauri wa Wizara ya Kamati ya Umoja wa Afrika ambayo inashughulikia masuala ya migogoro ya mafuta nchi za Waarabu.
Nyumbani kwake Masaki
Mazingira ya nyumbani kwa Sir Chande, Masaki hayaonyeshi eneo hilo kama kuna tukio lolote kubwa kutokana na ukimya uliokuwepo jana.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye alifika nyumbani hapo mchana, alishuhudia wana ndugu wachache pamoja na watoto waliokuwa ndani.
Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na waombolezaji wapatao watano waliokuwa wakionekana sebuleni huku baadhi ya wana ndugu wakitajwa kuwa eneo la juu la nyumba hiyo wakiendelea na kikao cha kupanga taratibu za mazishi.
Sir Chande alizaliwa Mei 7, mwaka 1928 nchini Mombasa, Kenya ameacha mjane Jayalaxmi na watoto watatu.
Hatua kwa hatua atakavyochomwa
Baada ya mwili wa marehemu kuingia ndani ya jengo lakuchomea maiti, Wahindi huvunja nazi tatu katika kaburi lililo karibu kabisa na lango kuu.
Baada ya hapo mwili huletwa katika tanuru lenyewe na hupangwa kuni juu ya tanuru hilo ambalo limeundwa mithili ya kitanda cha chuma.
Kuni hupangwa kwa ustadi mkubwa na zile za ukubwa kiasi hupangwa katika umbile la reli na magogo makubwa manne hupangwa kushoto, kulia Magharibi na Mashariki ya tanuru hilo ambapo kuni zinakuwa nyingi.
Kabla ya kuchoma maiti
Kabla ya kuuweka mwili katika tanuru huuzungusha mara nne kulizunguka tanuru hilo.
Baada ya hapo, mwili wa marehemu ukiwa na sanda huwekwa katikati ya kuni hizo, kichwa kikielekezwa Magharibi.
Kabla ya uchomaji wenyewe kuanza, mila za Wahindu hutaka kuhakikisha iwapo kweli ndugu yao amefariki.
Ndugu mmoja wa marehemu hutakiwa kuhakiki kwa kuchukua kipande kidogo cha kuni chembamba kilichoshika moto, kisha humchoma marehemu katika unyayo mara nne huku akilizunguka tanuru.
Hatua inayofuata ni kuchukua moto kwa kutumia makoleo maalumu, kisha kuuchanganya moto huo na mafuta ya samli.
Mwili wa marehemu hupakwa mafuta ya samli kuanzia usoni mpaka miguuni kabla ya kuwasha moto, baada ya hapo moto huwashwa na unakuwa moto mkali zaidi ya gesi.
Mafuta ya samli pamoja na mafuta ya marehemu mwenyewe husaidia moto kuwa mkali kuliko kawaida.
Wakati moto unaendelea kuwaka kwa kasi, mbegu za ufuta hurushwa juu ya mwili unaoendelea kuungua na ndugu za marehemu ambao wanakuwa wamelizunguka tanuru.
Uchomaji mwili kawaida huchukuwa saa mbili au mbili na nusu kumalizika au kuteketea kabisa.
Baada ya mwili kuungua na kwisha kabisa, kinachotakiwa kubaki ni vipande vya mifupa, lakini wakati mwingine moto huweza kwisha kabisa na wakati huo mwili bado haujamalizika.
Baada ya mwili kuchomwa na kwisha, ndugu mmoja wa marehemu huchukua chungu maalumu kilichojazwa maji na kukiweka katikati ya miguu, kisha anatakiwa kutazama Magharibi akiyapa kisogo mabaki ya mwili huo wakati huo waombolezaji wote wanageuka pia.
Anachofanya ndugu huyo wa marehemu akiwa amesimama ni kuchukua jiwe na kukipiga chungu hicho kwa nguvu hadi kivunjike na maji yamwagike kuelekea lilipo tanuru.
Baada ya tukio hilo yeye pamoja na umati wote wa waombolezaji hutakiwa kuondoka bila kugeuka nyuma.
Kwa upande mwingine baada ya mwili kuchomwa na moto kumalizika kabisa, mabaki ya mwili hutolewa kama vipande vya mifupa ya mwili na fuvu, vilivyochanganyika na majivu na mkaa kutoka tanuruni.
Mifupa hiyo huwekwa katika mifuko maalumu na hatua ya mwisho ni ndugu kwenda kuyatupa baharini.