Wednesday, 11 January 2017
Mbaroni kwa kumchapa mwanamke viboko 30
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya mkoani Mara, linawashikilia watu 10 kwa udhalilishaji wa kumchapa viboko mwanamke hadharani.
Watu hao ni wa kijiji cha Kinesi tarafa ya Suba wilayani Rorya. Miongoni mwa watu hao, wamo viongozi watano wa baraza la mila liitwalo Irienyi ndogo la kabila la Wasimbiti.
Watu hao wanatuhumiwa kumchapa viboko zaidi ya 30 hadharani mwanamke huyo, kitendo kilichomdhalilisha mbele ya jamii.
Mapema wiki hii, baadhi ya video ilisambaa katika mitandao ya kijamii, ikimuonesha mwanamke akichapwa viboko na wanaume kwa zamu huku akilia mbele ya hadhara na sauti za wanaume zilisikika zikishabikia kitendo hicho.
Kamanda wa Polisi Tarime/ Rorya, Andrew Satta alisema kuwa tukio hilo ni la Desemba 23 mwaka jana mchana katika kitongoji cha Migutu kijiji cha Kinesi tarafa hiyo ya Suba wilayani Rorya katika maeneo ya Mastooni, ambako kulikuwa na mkutano wa Ritongo wa mila.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa kijiji hicho (jina limehifadhiwa) aliitwa na kufuatwa na vijana na kupelekwa katika mkutano huo wa mila, uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa kijiji hicho. Ilidaiwa kuwa mwanamke huyo alimtuhumu mama yake mzazi wa umri wa miaka 55 kuwa ni mchawi.
Kwamba hamtambui na kumkana kuwa si mama yake mzazi; huku akidai kuwa mama huyo anataka kumuua kwa uchawi. Kamanda Satta alisema katika mkutano huo wa baraza la mila la Irienyi, vijana sita waliamriwa kumchapa kila mmoja viboko vitano makalioni mwanamke huyo, hali iliyomsababishia majeraha, kumuathiri, kumdhalilisha na kumshushia utu wake kwa jamii.
“Tumewakamata mwenyekiti wa baraza hilo, viongozi wenzake wanne na vijana sita walioshiriki kumkamata na kuadhibu kwa kumlaza chini, kumchapa viboko na kumsababishia madhara makubwa mwilini na kumdhalilisha,” alisema Kamanda. Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na jeshi hilo linaendelea kuwasaka wengine waliohusika.
MAMBO HAYA UKIYAFANYA UTAPONA VIDONDA VYA TUMBO HARAKA
Tatizo la vidonda vya tumbo si geni sana kwa watu kadhaa hapa nchini hata kama halijawahi kukupata wewe basi huenda rafiki yako au jirani utakuwa umewahi sikia akizngumzia.
Sasa hapa leo napenda kukwambia mambo kadhaa ambayo ukiyafanya yanaweza kukuweka mbali dhidi ya tatizo hilo au kupunguza madhara ya tatizo hilo.
1. Kuepuka kula mlo mkubwa kwa wakati mmoja na badala yake unaweza kula mara nyingi lakini kidogo kidogo. Hii itakusaidia upunguza madhara ya tatizo hilo.
2. Epuka kula muda mchache kabla ya kuelekea kulala na badala yake unapaswa kujitahidi kula angalau saa 3 hadi 4 kabla ya kuelekea kulala.
3.Acha kupuuza unywaji wa maji mengi, jaribu kunywa maji ya kutosha kila siku hii hupunguza dalili za tatizo hilo.
4. Punguza msongo wa mawazo kwani mawazo huchangia uzalishaji wa asid nyingi tumboni na baadaye kusababisha vidonda hivyo vya tumbo.
5. Acha kabisa kuvuta sigara na kunywa pombe ili kupunguza madhara ya tatizo hilo.
Kwa maelezo zaidi na ushauri tupigie kwa simu namba 0716 300 200/ 0769 400 800/ 0784 300 300 au barua pepe dkmandaitz@gmail.cm
Ushauri huu umetolewa chini ya Shirika lisilokuwa la Kiserikali la The Work Up Tanzania (WUTA) ambalo linadhamira ya dhati ya kupambana na umasikini, ujinga na maradhi kwa kuhamasiha matumizi ya lishe bora. Pia unaweza kufika ofisini kwetu Ukonga Mongolandege jijini Dar es Salam kwa ushauri zaid.
Bodi ya Mikopo yatua Precision, Mantrac na Pepsi
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) imeendelea kufuatilia waajiri wasiotekeleza sheria ya bodi ya kuwataka kupeleka makato ya wanufaika wa mikopo waliopo katika ofisi katika taasisi na kampuni mbalimbali Dar es Salaam.
Katika ufuatiliaji huo, jana bodi hiyo ilikwenda katika kampuni tatu, Kampuni ya ndege ya Precision, Kampuni ya Mantrac na kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi (SBC Tanzania Limited ).
Wakiwa katika ofisi za Precision, walishindwa kuonana na uongozi baada ya katibu muhtasi kukataa kutoa ushirikiano kwa madai hawakuwa na miadi na uongozi wa kampuni hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HELSB, Phidelis Joseph alisema, amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Precision.
Alisema licha ya kampuni hiyo kugoma kutoa ushirikiano, lakini wamekuwa na tabia ya kulimbikiza marejesho, jambo ambalo sio sahihi na kupeleka baadhi ya majina huku mengine wakiyaacha.
“Leo (jana) tumekosa ushirikiano wamegoma kuonana na sisi, kampuni hii ni moja ya ambazo zimekuwa na usumbufu na kushindwa kuleta marejesho kwa wakati wanapaswa kulipa Sh milioni saba kwa mwezi wameshindwa kufanya hivyo na kusababisha kuwa na deni la Sh milioni 31 kama faini kwa kuchelewa kupeleka marejesho kwa kipindi cha miezi 20,” alisema.
Aidha alisema idadi iliyotolewa na kampuni hiyo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumishi katika kampuni hiyo ambayo vyanzo vya bodi hiyo imebaini uwepo wa wanufaika wengine katika kampuni hiyo lakini majina yao hayajapelekwa na mwajiri katika bodi hiyo.
“Haiwezekani kampuni kama Precision iwe na wanufaika saba tu shirika zima, sisi tunatambua wapo zaidi ya hao saba tunachokitaka walete majina ya wanufaika wote na pia walete marejesho kwa wakati ili fedha hizo zitumike kwa wanafunzi wengine wanaohitaji kupata mkopo na kama wakishindwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria,”aliongeza.
Akiwa Pepsi, Joseph alisema, kampuni hiyo imekuwa ikisumbua kwa muda mrefu, kwani wametengeneza bili ya watu zaidi 45 waliorodheshwa kama wanufaika tangu Septemba mwaka 2015, lakini hawajapeleka fedha na kila mara wamekuwa wakiwasiliana na kiongozi wa kampuni hiyo, lakini amekuwa akionesha dharau bila kutoa ushirikiano, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Tunashangaa hapa makao makuu hawaleti fedha hizo lakini katika matawi yao ya Moshi na Arusha wamekuwa wakilipa tunataka leo wamtume mtu ofisini kwetu kuchukua majina ambayo tumeyaorodhesha na majibu ya kwanini wameshindwa kulipa kwa muda mrefu pamoja na majina halali ya wanufaika na wakishindwa tutawachukulia hatua,”alisema.
Katika Kampuni ya Mantrac, Joseph alisema kampuni hiyo imeonekana kuorodhesha majina machache, ili hali vyanzo vya bodi hiyo vinafahamu uwepo wa wanufaika wengine wanaofanya kazi hapo.
Pia alisema kampuni hiyo imeshindwa kulipa marejesho tangu mwezi Julai mwaka jana, hivyo amewataka kuhakikisha wanalipa malimbikizo hayo kwa wakati ili kuepuka faini.
“Tumezungumza na Meneja rasilimali watu na tumemueleza ameahidi kufuatilia na kuhakikisha wanaleta marejesho ambayo wameyalimbikiza kwa wakati na kufuatilia kuona kama kuna wanufaika zaidi walioajiriwa lakini majina hayajatufikia,”aliongeza.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa bodi hiyo, Wambura Mkono alisema, waajiri wanatakiwa kuwasilisha majina ya wafanyakazi wao ndani ya siku 28 baada ya kuwaajiri ili waweze kuwaangalia endapo ni wanufaika au la; na atakapojulishwa kuwa ni wanufaika, anatakiwa kumkata asilimia 15 ya mshahara wake na kuiwasilisha bodi ya mkopo kabla ya tarehe 15 ya mwezi unaofuata katika kalenda.