K
Muda mfupi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaita polisi kuhojiwa kwa tuhuma mbalimbali, baadhi ya walioitwa wamelaani hatua hiyo wakisema inalenga kuwachafulia majina na heshima mbele ya jamii.
Miongoni mwa waliotwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye amezungumza na kueleza kutofurahishwa na hatua hiyo.
Mbowe aliyekuwa safarini kwenda bungeni Dodoma, alisema ameshangazwa kutuhumiwa kwa jambo asilolijua.
“Kama amemtaja mbunge wa Hai anajulikana ni mmoja, hata kama asingesema Freeman, Mbunge wa Hai anajulikana ni Freeman Mbowe.
“The only thing (kitu pekee) ninaweza kusema nchi haiendeshwi hivyo. Yametajwa majina mengi ambayo sijui Makonda ana evidence (ushahidi) gani!
“Anasema tukiwaita tukiridhika na maelezo yao tutawaachia. Huwezi kusema tu, yaani kwa kusema ni Mbowe... mimi ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mimi ni mbunge, mimi ni mzazi, nina wanachama, maaskofu, mapadri, mashehe na viongozi mbalimbali.
“Unapokuwa unamhusisha kiongozi na ‘drug trafficking au drug business’ (usafirishaji wa dawa au biashara ya dawa za kulevya), sijui ana ushahidi gani hadi akanihusisha na jambo hilo, mimi sielewi, kwa hivyo siwezi kusema kwa kitu ambacho sielewi,” alisisitiza Mbowe.
Mbowe aliendelea kusema kuwa kesi za dawa za kulevya hazina dhamana, hivyo alimtaka Makonda awe na ushahidi wa kutosha anapowataja watuhumiwa.
“Tuache habari ya kuitwa, wewe umepata tuhuma, hujafanya uchunguzi, hakuna mtu aliye juu ya sheria, lakini unatakiwa kufanya uchunguzi ili ukimkamata mtu unamshtaki, siyo unataja mtu unachafua hadhi yake. Halafu ukija kusema hatuna ushahidi juu yako umeshaharibu jina lake,” alisema na kuongeza:
“Mimi sijui kama jeshi la polisi linafanya kazi hii au ni Makonda amejipa kazi ya kuwa mpelelezi. Au labda yeye kwa kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ndiyo amejipa kazi ya kutaja majina kwenye mambo yenye kashfa kama haya? Sielewi. This is very wrong precedence (Hii ni rejea mbaya) kwa utawala wa sheria.”
Mbowe alisema inawezekana ni mikakati ya Serikali kuendelea kukandamiza upinzani kwa kuwakamata viongozi wake.
“Sijui kama kuna watu wanaolengwa, lakini tumeona viongozi wetu wanakamatwa hawapewi dhamana, (Tundu) Lissu amekamatwa, (Godbless) Lema amekamatwa ... mtu anakaa miezi minne, kwa hiyo wanaweza kufanya lolote. Inawezekana ni mkakati wa kutesa wapinzani. Wamenitafuta kwenye biashara wameona haitoshi... sina uhakika lakini sioni kama wana nia njema na sisi,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa kama ataitikia wito wa Makonda, Mbowe alisema bado anawasiliana na wanasheria wake kabla ya kuchukua hatua.