DODOMA: Serikali imetoa nafasi kwa watumishi wanaodhani kuwa wameonewa, baada ya kutajwa kwenye orodha ya watumishi wenye vyeti vya kugushi (feki) waandike barua ya kukata rufaa na kwa katibu mkuu wa wizara ya utumishi kuanzia kesho ili malalamiko yao yashughulikiwe haraka.
Hatua hiyo imefikiwa leo Bungeni baada ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela kuomba mwongozo wa spika kuhusiana na suala la baadhi ya watumishi kudai kuwa wameonewa kwenye sakata hilo.
Akitoa mwongo huo, Kunchela amesema kuwa sakata la vyeti feki limeibua malalamiko mengi miongozi mwa watumishi waliokumbwa na suala hilo huku wengine wakidaiwa ‘kuchanganyikiwa’ na kupoteza mwelekeo wa maisha.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki amelieleza Bunge kuwa, serikali imewapa nafasi watumishi wote wanaodhani kuwa wameonewa kwenye sakata hilo basi waandike barua za rufaa ya malalamiko yao na waiwasilishe kwa katibu mkuu wa wizara hiyo ili malalamiko yao yashughulikiwe mapema.
“Kwa wale ambao wanafahamu kabisa kwamba vyeti vyao ni vya kugushi, wasithubutu kukata rufaa kwa kuwa ikibainika tena kwamba wamefoji, hatua kali zaidi zitachukuliwa.” Alisema Kairuki.