Thursday, 29 September 2016
MWALIMU JELA MIAKA 32 KWA KUMNAJISI NA KUMPA UJAUZITO MWANAFUNZI WA DARASA LA NNE
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imemhukumu Mwalimu wa Shule ya Msingi Ukingwamizi, Une Thom kutumikia kifungo cha miaka 32 jela.
Thom (32) amehukumiwa kifungo hicho baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani kwa makosa mawili ya kumnajisi na kumpatia ujauzito mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka 16. Msichana huyo ambaye amejifungua mtoto njiti aliyekufa baada ya kuzaliwa, alikuwa akisoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Ukingwamizi , Kata ya Mamba wilayani Mlele mkoani Katavi.
Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Teotimus Swai kwa kuwa adhabu hizo zinaenda sambamba, mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Swai amesema mahakamanikuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, Baraka Hongoli umethibitisha kuwa kweli mshtakiwa alitenda kosa hilo.
“Nimetoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa ili iwe fundisho sio kwako tu bali pia kwa wengine wenye tabia kama yako, kosa la kunajisi adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela. Na kosa la pili la kumpatia mwanafunzi huyo ujauzito kifungo chake ni miaka miwili jela. Hivyo kwa pamoja utatumikia kifungo cha miaka 30 jela,”alisema.
Mwendesha mashitaka, Mkaguzi wa Polisi, Baraka Hongoli alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi wake huyo kwa muda mrefu hadi akamsababishia ujauzito.
Imeandikwa na Peti Siyame- Habarileo