KUANGALIA MKOPO WAKO
<<BONYEZA HAPA>>
HABARI KARIBU YAKO ZAIDI.
RAIS John Magufuli amebubujikwa na machozi hadharani wakati akiongoza mamia ya waombolezaji jijini Dar es Salaam, kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri katika awamu nne za uongozi wa nchi na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai, aliyefariki ghafla Novemba 8, mwaka huu.
Mbali na Dk Magufuli, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mke wa Rais mstaafu Mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk Mohamed Gharib Bilal, mawaziri wakuu wastaafu Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva, mawaziri na viongozi wengine mbalimbali walitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mungai, katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana.
Baada ya shughuli hiyo, mwili wa Mungai ulipelekwa nyumbani kwake Osterbay kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kwa maziko, yatakayofanyika kesho.
Kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga, alimwelezea Mungai kuwa alikuwa na kipaji cha tofauti cha uongozi tangu akiwa mdogo.
“Uongozi pekee ni tunu. Mungai alikuwa na sifa ya uongozi. Lakini kipindi cha uongozi ni jinsi unavyotafsiri uongozi wako kwa wale unaowaongoza. Alitumia kipaji chake cha uongozi kwa jamii,” alisema Balozi Mahiga na kubainisha kuwa baba mzazi wa marehemu alitokea Kenya na mama yake mzazi alitoka katika ukoo wa Chifu Mkwawa.
Naye mtoto wa marehemu, Jim Mungai, alisema baba yake alikuwa Mbunge kwa miaka 35 katika Jimbo la Mufindi na baadaye baada ya kugawanywa Mufindi Kaskazini.
Alisema katika miaka yake hiyo kwa awamu nne alikuwa Waziri wa Kilimo, Elimu, Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM. Alisema ameacha mke na watoto saba.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Sumaye alimwelezea Mungai na kusema kuwa katika kipindi chake cha uwaziri, alikuwa waziri wa elimu mchapakazi, mwadilifu na kwamba aliongoza wizara hiyo vizuri hadi viwango vya elimu viliongezeka.
“Tumempoteza mtu muhimu sana katika nchi,” alisema Sumaye.
Aliyekuwa Waziri katika Awamu ya Nne, Steven Wassira alisema alifanya kazi na Mungai katika wizara moja ya kilimo, akiwa Naibu Waziri wake wa Kilimo.
Aliongeza kuwa Mungai alipenda kuona mabadiliko ya kilimo katika sekta zote ndio maana karibu awamu zote nne aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru alimwelezea Mungai kuwa alikuwa mtu aliyekuwa na kichwa kizuri katika utendaji kwa kuwa katika nafasi zote alizopewa alikuwa mchapakazi.
“Alikuwa akitoa mchango bungeni alioufanyia utafiti wa kina na unakuwa ni wa kujenga,” alisema. Serikali imemteua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuiwakilisha kwenye maziko yatakayofanyika kesho.
Rais wa Marekani, Barack Obama leo amekutana na Rais Mteule wa nchi hiyo, Donald Trump ambapo wamefanya mazungumzo baina yao wawili kuhusu mambo mbalimbali ya nchi hiyo na baada ya hapo kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa wamejitokeza kwa wingi katika Ikulu ya Marekani ‘White House.’Trump na Mkewe waliwasili katika Ikulu ya Marekani saa nne unusu asubuhi (saa za Marekani) na kutumia mlango wa nyumba ambao waandishi wa habari hawakuweza kumuona akiingia.
Wakizngumza na waandishi wa habari, Barack Obama amesema kuwa amekuwa na mazungumzo mazuri na Donald Trump ambapo wamezungumzia kuhusu masuala ya sera za mambo ya nje, mambo ya ndani na masuala ya ulinzi na kubwa kuhusu makabidhiano ya ofisi yatakayofikia tamati Ijumaa, Januari 20, 2017 wakati Trump atakapoapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani.
Kwa upande wa Trump alisema kuwa ni furaha kwake kukutana na kuzungumza na Rais Obama kwa mara ya kwanza na anatarajia kukutana na kushirikiana naye mara nyingi zaidi.
Kwa upande wa mke wa Trump, yeye amekutana na mke wa Rais Obama, Michelle Obama ambao nao wamefanya mazungumzo kuhusu ofosi ya Mama wa Taifa (First Lady).Hapa chini ni picha za Rais wa Marekani na Rais Mteule wa Marekani wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao.
ASKARI wawili waliofukuzwa kazi na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya wamepandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mkoa wa Mbeya wakikabiliwa na jumla ya mashitaka 13 waliyoyatenda dhidi ya wanafunzi wa kidato cha nne likiwamo la kuwaingilia kimwili kwa nguvu.
Waliopandishwa kizimbani ni Konstebo Petro Magana aliyekuwa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mbeya na Konstebo Lucas Ng’weina wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
Katika kesi namba 147 ya mwaka 2016, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Catherine Paul mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo Novemba 4, mwaka huu saa tano usiku katika Shule ya Sekondari Isuto iliyopo wilayani Mbeya.
Mwendesha Mashitaka aliiambia mahakama hiyo kuwa katika shitaka la kwanza la kosa la udhalilishaji wa hali ya juu linalomkabili Konstebo Petro pekee, siku ya tukio mshitakiwa alijaribu kumwingilia kimwili mwanafunzi (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 14 huku pia akimdhalilisha mwanafunzi huyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria Kifungu namba 138 A cha Kanuni ya Adhabu.
Alisema kwa shitaka la pili la kosa la udhalilishaji wa hali ya juu pia linalomkabili Konstebo Lucas peke yake, siku ya tukio mshitakiwa alijaribu kumwingilia kimwili mwanafunzi (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 16 na kisha kumdhalilisha jambo ambalo pia ni kinyume cha sheria Kifungu namba 138 A cha Kanuni ya Adhabu.
Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali alizidi kubainisha kuwa mashitaka mengine yote kuanzia shitaka namba tatu hadi 13 yanayohusu shambulio yanawakabili washitakiwa wote wawili kwani kwa pamoja waliwashambulia wanafunzi 11 wa kidato cha nne kwa kuwachapa viboko sehemu mbalimbali za miili yao jambo ambalo ni kinyume cha Sheria Kifungu cha 240 cha Kanuni ya Adhabu.
Aliwataja wanafunzi walioshambuliwa na askari hao kuwa ni Neema Mabalanjo, Vicky Mwaya, Tumpe Jonas, Ombeni Tuonee, Lutabite Landa, Jane Msukulu, Zulfa Julius, Atupole Boniface, Betha Joseph, Blandina Mwaigaga na Zainabu Leonard.
Hakimu Mkazi Laizer aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, huku akisema dhamana kwa washitakiwa wote wawili iko wazi kwa masharti ya kila mmoja kutosafiri nje ya Mkoa wa Mbeya bila idhini ya mahakama hiyo na pia kila mshitakiwa kuleta mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa umma ambaye ataweka dhamana ya malikauli isiyopungua thamani ya Sh milioni saba.
Hadi kesi hiyo inaahirishwa mahakamani hapo washitakiwa wote ambao kwa pamoja wanatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Josephat Kazeula walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kutakiwa kurudishwa rumande.