WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewatangazia kiama watu wote waliohusika kuwaua askari polisi nane Kibiti wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari hao jijini Dar es Salaam leo asubuhi Mwigulu alisema watu hao watakamatwa wote na kufikishwa kwenye mkono wa sheria.
"Kitendo hiki cha mauaji kilichofanyika dhidi ya askari wetu hakivumiliki hata kidogo waliohusika tutawatafuta na kuwakamata" alisema Mwigulu.
Aliwaomba wananchi wa maeneo husika kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwapata wahusika wa tukio hilo.
Katika hatua nyingine Mwigulu ameitaka wizara husika kuhakikisha inatoa fidia kwa ndugu wa askari hao na majeruhi badala ya kuchukua muda mrefu kuitoa.
"Naomba fidia kwa askari hawa tuliowapoteza wakitumikia taifa itolewa haraka bila kucheleweshwa" aliongeza Mwigulu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu alisema watuhumiwa wote waliohusika kufanya mauaji hayo ni lazima watafikiwa na mkono wa dola.
Alisema wananchi wa eneo hilo wanawafahamu wahusika hivyo amewaomba washirikiane na polisi ili kuwapata vinginevyo nguvu itatumika.
Alisema linapotokea tukio kama hilo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakishabikia kupitia mitandao ya kijamii hivyo akatoa onyo kuwa watakao bainika na wao watakamatwa kwa kutenda kosa.
Askari waliopoteza maisha katika tukio hilo la kinyama wametajwa kuwa ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub.