Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imeongeza muda wa udahili wa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu mwaka wa masomo 2016/2017 ili kuwapa fursa waombaji ambao wana sifa lakini hawakupata vyuo kutokana na ushindani wa vyuo na kozi walizozichagua.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Eleuther Mwageni alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya mwenendo mzima wa udahili kwa mwaka wa masomo 2016/2017, leo Jijini, Dar es Salaam.
“ Tume imekamilisha awamu ya kwanza ya udahili kwa waombaji wenye sifa ya kidato cha 6, ambapo jumla ya waombaji wote ilikuwa 55,347, waombaji wenye sifa ni 47,203 sawa na asilimia 85.3 ya waombaji wote. Katika waombaji hao wenye sifa waliopata vyuo ni 30,731 sawa na asilimia 65 na waombaji 16,472 ambao wana sifa sawa na asilimia 35 hawajapata vyuo hadi sasa, waombaji waliokosa sifa ni 8,144,” alifafanua Prof. Mwageni.
Amesema kuwa Tume imeamua kuongeza muda wa udahili kuanzia Septemba 12 mpaka Septemba 23, 2016 ili kuwapa nafasi waombaji wenye sifa, fursa ya kuomba tena vyuo na kozi zenye nafasi kutokana na wengi wao kuomba vyuo na kozi za aina moja.
Prof. Mwageni alivitaja vyuo ambavyo vimeombwa na waombaji wengi na tayari vimeshajaa kuwa ni Chuo cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi, Chuo Kikuu cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro(KCMUCo) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.
Pia alizitaja kozi ambazo zimechaguliwa na waombaji wengi kuliko nafasi zilizopo kuwa ni kozi ya Ualimu, Udaktari wa Binadamu, Ufamasia, Uhandisi, Sayansi ya Uthamini wa Ardhi na Sheria. Alitoa mfano wa kozi ya Ualimu Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam ilikuwa na waombaji 15,803 wakati nafasi ni 1,000.
Hivyo amewashauri waombaji waliokosa nafasi kuomba vyuo na kozi zisizo na ushindani ili waweze kupata nafasi kwa awamu hii ya pili.
Aidha Tume hiyo imepunguza viwango vya udahili kwa waombaji wenye sifa ya stashahada kutoka GPA 3.5 mpaka 3.0. Hivyo wamewataka waombaji wenye vigezo hivyo kuomba vyuo na kwa wale waliomba awamu ya kwanza hawatatakiwa kuomba tena bali kusubiri matokeo ya waombaji wenye sifa ya stashahada.