MKUU wa wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Ali Hapi, ametoa onyo kwa wamiliki wa baa wanaowahifadhi watu wanaojihusisha na biashara ya ngono ‘Machangudoa’ kuwa watafutiwa leseni.
Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kata ya Kijitonyama waliodai kuwa kuna baadhi ya baa zimekuwa zikiwahifadhi wanaouza miili, hali ambayo ni hatari kwa mazingira na makuzi ya watoto.
Hapi amesema haiwezekani serikali iwe inapambana na biashara hiyo haramu lakini kuna baadhi ya baa zinawafuga machangudoa.
"Tutashughulika na changudoa na tutashughulika na wenye baa zinazowahifadhi machangudoa, kwa sababu hili ni suala lililo kinyume cha sheria, serikali inapambana na hili tatizo halafu mwingine analikumbatia, hilo haliwezekani, tutawachukulia hatua za kisheria," amesema.
Awali, akitoa malalamiko yake kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete, mkazi wa Kijitonyama alidai kuna baa zilizogeuka kero kwao.
Ameitaja baa iitwayo Kona ya Sinza imekuwa ikiwahifadhi machangudoa hivyo kuhatarisha makuzi ya watoto kwa kuwa wanaweza kuiga tabia zisizofaa.
"Hii baa iko hapo Afrika Sana, machangudoa wako pale wanajiuza hadharani, sasa kwa kweli hii ni kero kubwa kwetu, watoto wanaweza kuiga na matokeo yake tutakuwa na kizazi kibaya ," amesema mwananchi huyo.
0 comments:
POST A COMMENT