Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine leo | KINGAZI BLOG

HABARI KARIBU YAKO ZAIDI.

Breaking News
Loading...

Tuesday, 4 April 2017

Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine leo



TUJIKUMBISHE HISTORIA YAKE 

Prof. Kitila Mkumbo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa. Alizaliwa tarehe 21 Juni 1971 katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba, Singida. Prof. Kitila hakuwa na bahati ya kulelewa na wazazi, hivyo alisomeshwa kwa misaada ya ndugu na wasamaria wema.

Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko wilaya ya Iramba kati ya mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya Sekondari Mwenge (Singida) na kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1988-1991 na elimu ya Juu ya Sekondari akaipata pale Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka 1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).

Baada ya kuhitimu kidato cha sita alifanya kazi ya kuvua samaki katika Bwawa la Mtera huko Iringa kwa sababu ya kuwa na hali mbaya ya kiuchumi na baadaye alipata nafasi ya kwenda kujiunga na mafunzo ya polisi kwenye Chuo cha jeshi CCP Moshi kwa muda wa miezi miwili lakini alikatisha mafunzo baada ya kuchaguliwa kujiunga Chuo Kikuu.

Prof. Kitila alihitimu shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1999 akisomea Sayansi ya Elimu akaanza kazi hapo hapo Chuo Kikuu kama Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 – 2003) na wakati anafanya kazi aliendelea kusoma shahada ya uzamili/umahiri (M.A) akibobea katika Saikolojia, alihitimu shahada hiyo mwaka 2002.

Kitila alifanya vizuri katika shahada ya umahiri na baada ya kufundisha Chuo Kikuu kwa miaka michache alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha Southampton kilichoko nchini Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya uzamivu akibobea pia katika saikolojia, hii ilikuwa ni mwaka 2008.

Kati ya mwaka 2009 – 2012, Prof. Kitila amefanya kazi kama mratibu wa kamati ndogo ya ufundi ya masuala ya UKIMWI lakini pia kuanzia mwaka 2010 hadi hivi sasa ameendelea kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCIB (Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB).

Mwaka 2010 hadi 2012 amekuwa Makamu Mwenyekiti wa UDASA (Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam) na kisha akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UDASA Oktoba 2014 na anaendelea na wadhifa huo.

Mwaka 2009 alikuwa Ofisa anayesimamia mitihani katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, amekuwa mhariri mkuu na mhariri msaidizi wa machapisho mbalimbali yanayohusu elimu ya saikolojia, sanaa na sayansi.

Pia, amekuwa mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na masomo ya Mtaala katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaama kuanzia mwaka 2009 – 2012, amekuwa Mhadhiri Mwandamizi kuanzia mwaka 2011 – 2014, amekuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Cha Elimu cha Dar Es Salaam (DUCE) na kufanikiwa kuwa Profesa Mshiriki katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuanzia Julai 2014.

Kitila alianza siasa kama mwanachama wa CCM, baadaye alijiunga CHADEMA kawa mshauri muhimu wa chama hicho. Naweza kuthubutu kusema, kati ya wasomi na wataalam waliotoa mchango mkubwa kiushauri, kiuhaulishaji na kimkakati na kuifanya CHADEMA iwe chama kinachojiendesha kisasa sana leo hii, mmoja wa wasomi hao ni Prof. Kitila.

Mwaka majuzi  (2014), Prof. Kitila alifukuzwa katika chama chake cha zamani (CHADEMA) kwa tuhuma za kuandaa waraka wa mapinduzi na kukihujumu chama hicho, Kitila alitangaza kuwa angeshirikiana na wenzake kuanzisha chama kipya ambacho hivi sasa kinajukana kama ACT – Wazalendo. Na hata rafiki yake wa siku nyingi, Zitto Kabwe amekweishjiunga na chama hicho. Hata katika chama hiki kipya yeye amekuwa mshauri mkuu. Watu nilioongea nao kutoka ndani ya ACT wanasisitiza kuwa Kitila ana mchango mkubwa na unaoonekana anapokuwa katika taasisi yoyote ile.
Prof. Kitila amekwishafanya tafiti zaidi ya 18 na zimechapishwa katika majarida ya kitaaluma ya kimataifa, amekwishaandika vitabu takribani vitatu, ameoa na ana watoto watatu.

MBIO ZA UBUNGE

Prof. Kitila hakuwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote hapa Tanzania, muda wake mwingi amejikita katika masuala ya kitaaluma na ushauri wa mikakati ya kisiasa. Japokuwa alipokuwa mwanachama hai wa CHADEMA alifanya harakati nyingi katika jimbo la Iramba, (jimbo linaloongozwa na Mwigulu Nchemba wa CCM) na amewahi kuingia kwenye misukosuko mingi na hata kufunguliwa kesi ya kisiasa kwa sababu ya harakati zake.

NGUVU YAKE

Sifa na nguvu ya kwanza ya Prof. Kitila ni kuwa kijana na msomi mahiri. Pamoja na kuwa wasomi wengi wanapewa madaraka na wanavurunda kama vile hawakwenda shule, bado mataifa yote duniani hayakwepi wala kukimbia dhana ya kuongozwa na watu walioelimika maana kuna wasomi wengi tu ambao ni waadilifu sana katika kazi zao, mmoja wao ni Prof. Kitila. Ukiniuliza mmoja kati ya wasomi wanaojua majukumu yao na wanayasimamia sana, ntakwambia Prof. Kitila ni mmoja wao. Nguvu na sifa hii vina maana kubwa sana kwa mtu ambaye anafikiri au anafikiriwa kuwa rais wa nchi.Lakini jambo la pili, yeye ni mwanademokrasia thabiti na anayependa demokrasia iwe katika vitendo. Msomi huyu ni mmoja wa watu wanaoamini katika kujenga hoja na wanaopenda hoja zishindanishwe na zijadiliwe kwa uwazi na kisha hoja yenye mashiko ndiyo ipitishwe na kukubaliwa na pande zote kwa sababu ina tija kwa jamii au taifa.

Ukitembelea ukurasa wake wa “Facebook” utaona watu wanaandika jambo lolote na humuoni akigombana nao, anapingwa waziwazi na wakati mwingine anatukanwa lakini anaacha uhuru wa wanaompinga na kumtukana uendelee. (Mimi binafsi nimekuwa sipendi mtu anitukane au anidhalilishe kwenye mitandao, napenda kupingwa kwa hoja na si kutukanwa, na nakumbuka kila aliyenitukana niliishia kumuondoa miongoni mwa marafiki).

Prof. Kitila yeye ameenda mbali zaidi, yuko tayari kwa hoja na yuko tayari hata kutukanwa na kudhalilishwa, mwisho wa siku kila mtu huendelea kuwa rafiki yake kwa muktadha huo. Sifa hii ni ngumu mno kuipata kwa wanasiasa wengi, uvumilivu wao una ukomo lakini kwa Kitila ni tofauti. Nchi kama yetu inahitaji watu wa namna hii kwenye uongozi wa juu.

Jambo la tatu ambalo ni nguvu na sifa ya Prof. Kitila ni kubahatika kuwa kiongozi kila alipokaa, kusoma, kufanya kazi n.k. Amebahatika kuwa kiongozi tokea akiwa mdogo, nidhamu na kuwajali wenzake viliwavuta watu waliomzunguka kumtumia yeye awe mwakilishi wao. Amekuwa “kiranja” tokea akiwa Shule ya Msingi, Sekondari na Sekondari ya Juu. Uwezo huu wa kiuongozi uliendelea hata alipokuwa Chuo Kikuu (UDSM) kwani alichaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) kati ya mwaka 1998 – 1999.Watu nilioongea nao kuhusu uongozi wa Kitila alipokuwa DARUSO wananiambia alikuwa na karama za kipekee. Mmoja ambaye hivi sasa ni kiongozi mkubwa CCM na aliwahi kumpinga Kitila walipokuwa Chuo Kikuu, amenieleza kuwa Kitila alikuwa na ushawishi mkubwa kila akisimama mbele ya wanafunzi, hata kama mambo yalikuwa yemeharibika sana yalitengemaa. Kitila ni mmoja wa Marais wa DARUSO waliovuka vikwazo vya kutopinduliwa, watu waliowahi kuongoza DARUSO wanajua namna ilivyo rahisi sana kulala ukiwa Rais wa wanafunzi na ukaamka ukiwa Mwanafunzi wa kawaida.

UDHAIFU WAKE
Moja ya mambo ambayo nayatizama kama udhaifu mkubwa wa Prof. Kitila ni uthubutu unaopita kiasi. Binadamu waliofanikiwa huthubutu kufanya mambo kadha wa kwadha lakini uthubutu kwa kiwango kisicholeta madhara kulingana na mahali walipo. Jambo hili halifanywi na Kitila na mara kadhaa amethubutu kufanya mambo yaliyowagutusha wenzie.<br /><br />Mathalani, alipokuwa mwanachama wa CHADEMA alikiri kuhusika katika kuandaa waraka uliopewa jina maarufu la “waraka wa mapinduzi ndani ya CHADEMA”. Waraka ule ulikuwa ni moja ya mikakati ya msomi huyu kumpigia chapuo rafiki yake wa siku nyingi “Zitto Kabwe” ili ajiandae kuongoza chama hicho kupitia kwenye uchaguzi uliokuwa ukifuata. Waraka wa Kitila na wenzake ulitafsiriwa kama njama za mapinduzi ndani ya chama, usaliti na “kitu kisichofaa”.Uthubutu huu wa Kitila ungewezekana sana kama angekuwa anafanya kazi katika vyama vikubwa mno duniani, siyo hapa Afrika Mashariki, tena nchini Tanzania. Lazima tukubali kuwa vyama vya kiafrika vimejijenga katika mifumo migumu sana kuingilika kidemokrasia na mara nyingi vina shida kwenye eneo hilo, ndiyo maana nilishtushwa na kujua kwamba Kitila amekubali kuhusika na waraka ule wakati anatambua kuwa yuko Afrika ambako demokrasia inapiganiwa kwa matakwa ya walioko madarakani kwa wakati husika.Kwa siasa za Afrika, hata huko ACT ambako Kitila ni mwanachama leo hii, ukijaribu kuandaa waraka kama ule wa CHADEMA, nako unaweza kuonekana kama Msaliti, mfanya mapinduzi, mhaini n.k. Ndiyo maana nasisitiza kuwa uthubutu huu unaopitiliza ni tatizo kubwa sana kwake na kwa watu waliomzunguka na tamaduni zao. Hata akiwa Rais wa nchi atazungukwa na watu mbalimbali, aliowakuta na watakaomkuta, atakuwa na jukumu la kufanya mambo kwa uthubutu wa viwango vinavyokubalika ndani ya taasisi aliyomo kuliko “kuthubutu kulikovuka mipaka” ambako kunatizamwa kama uhaini kwa tamadani na demokrasia ya Afrika.Lakini kuthubutu huku kulikopitiliza ndiko pia kumemfanya Kitila mara kadhaa atofautiane sana na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwenye mambo kadha wa kadha. Ubishi, na kutokukubali mambo kirahisi au kutokukubaliana na mazingira na tamaduni za mahali ulipo, ni mambo ambayo yanamgharimu sana na nayatizama kama madhaifu yatakayoendelea kutishia ustawi wake kisiasa.Mchambuzi ni Julius Mtatiro, Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB (Student)



google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

    0 comments:

    POST A COMMENT

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us