New York. Donald John Trump alizaliwa Juni 14, 1946 Jamaica Estates, Queens karibu na New York. Ni mtoto wa pili kati ya watoto watano wa Fred Trump na Mary. Ndugu zake watatu; Maryanne, Elizabeth na Robert wako hai wakati kaka yake mkubwa, Fred Junior alifariki mwaka 1981 kutokana na unywaji pombe wa kupitiliza. Donald anasema jambo hilo ndilo lililomfanya yeye kujiepusha na pombe na uvutaji sigara.
Baba yake Trump kwa asili ni Mjerumani wakati mama yake asili yake ni Scotland. Bibi na babu zake Trump wote ni watu waliozaliwa Ulaya. Jina lao la asili la Kijerumani ni Drumpf baadaye katika karne ya 17 ndiyo likawa Trump. Trump anasema anajivunia asili yake.
Trump alizaliwa na kukulia mjini New York, alipata shahada yake ya kwanza ya uchumi katika shule ya uchumi ya Wharton ya Chuo Kikuu cha Pennyslvania mwaka 1968.
Mwaka 1971 alikabidhiwa udhibiti wa kampuni ya ujenzi ya baba yake Fred Trump ambayo baadaye aliibadilisha jina na kuiita The Trump Organization. Trump ni mwenyekiti na Rais wa Jumuiya ya Trump ambayo ni kampuni tanzu ya ujenzi, wadhifa ambao alisema atauacha mara atakapochaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Katika sekta ya ujenzi Trump amejenga ofisi, hoteli, casino na viwanja vya golf katika sehemu mbalimbali.
Mwaka 1996 hadi 2015, Trump alikuwa muandaaji wa mashindano ya urembo ya Miss USA na hapo pia akawa anaonekana katika filamu na vipindi mbalimbali vya runinga.
Mwaka 2016 aliorodheshwa katika jarida la Forbes kuwa mtu wa 324 kwa tajiri duniani, lakini anashika nafasi ya 156 ya utajiri nchini Marekani.
Ujana wake
Familia ya Trump ilikuwa na nyumba ya ghorofa mbili huko Wareham Jamaica Estates ambako Trump alikuwa akiishi wakati anasoma shule ya The Kew-Forest. Kutokana na tatizo la kimaadili, Trump aliacha shule akiwa na miaka 13 na kupelekwa chuo cha kijeshi cha New york (New York Military Academy - NYMA) ambako alimaliza sekondari mwaka 1983.
Baba yake (Fred Trump) wakati alipohojiwa kuhusu tabia za mwanawe alisema: “Donald alikuwa mkorofi alipokuwa mdogo.”
Mwaka 2015 Trump alimwambia mwandishi mmoja kuwa NYMA imempa mafunzo mengi ya kijeshi kuliko mtu yeyote aliyeingia jeshini.
Trump alisoma Chuo Kikuu cha Fordhan kwa miaka miwili kuanzia Agosti 1964 na kuhamia shule ya biashara katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania ambacho hutoa mafunzo kuhusu usimamizi wa ujenzi. Wakati akiwa chuoni hapo alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya familia iliyojulikana kama Elizabeth Trump & Son, jina la bibi yake mzaa baba.
Mwekezaji majengo
Trump hakuandikishwa kupigana vita ya Vietnam, lakini kati ya 1964 hadi 1968 akiwa chuoni alisimamishwa masomo mara nne.
Kuanza kazi
Trump alianza kazi katika kampuni ya baba yake mara tu baada ya kumaliza chuo. Kampuni hiyo ilikuwa ikijenga nyumba za makazi na kuzikodisha huko Brooklyn, Queens na Staten Island. Mradi wake wa kwanza aliousimamia ulikuwa ni kuboresha makazi ya Swifton Village apartment huko Cincinnati, Ohio sehemu ambayo ilinunuliwa na baba yake kwa dola 5.7 milioni mwaka 1962.
Donald na baba yake walisimamia mradi huo uliokuwa na uwekezaji wa dola 500,000 na kuweza kujenga nyumba 1,200. Trump anasema wakati anahitimu chuo mwaka 1968 alikuwa na utajiri wa kiasi cha dola 200,000 (sawa na dola 1,020,000 kwa mwaka 2015).
Mradi wa kwanza mkubwa wa Trump ulikuwa ni ujenzi wa Grand Hyatt Hotel mwaka 1978.
Mwaka 1981, Trump alinunua na kukarabati jengo huko Third Avenue mjini New York ambalo kwa sasa linajulikana kama Trump Plaza.
Mwaka 1983, Trump alikamilisha ujenzi wa Trump Tower yenye ghorofa 58 iliyopo Midtown Manhattan. Mwaka 1978 wakati Trump ananunua eneo hilo na kuweka mipango yake ya ujenzi kulikuwa na sintofahamu na majirani zake, ikabidi majadiliano yawe makali kwanini anataka kujenga jengo refu na kuwanyima haki ya eneo la anga jirani zake. Majadiliano yalipomalizika mwandishi mmoja wa The New York Times aliandika: “Trump alifanikiwa kulipata eneo… huo ni ushuhuda wa jinsi alivyo king’ang’anizi na uwezo wake wa kujadili na kufikia mwafaka.
Ndoa za Trump
Trump ameoa mara tatu na ana watoto watano na wajukuu wanane.
Mke wa kwanza wa Trump alikuwa ni Ivana. Huyu alikuwa ni mwanamitindo kutoka Jamhuri ya Czech, alimuoa mwaka 1977 na kuzaa naye watoto watatu: Donald Trump Jr, Ivanka na Eric. Ndoa hii ilivunjika rasmi 1992.
Ivana alizungumza na New York Post na kusema kwa sasa yeye na Trump ni marafiki na mara nyingi amekuwa akimshauri kuhusu hotuba zake. “Tulikuwa tunazungumza kabla na baada ya mikutano yake na alikuwa akiniuliza nafikiri nini? Nami humuambia kuwa atakuwa rais mzuri kwa sababu anasema kila kitu kama kilivyo.”
Aliyekuwa mke wa pili wa Trump ni Marla Maples, alimuoa 1993 na mwaka huohuo walipata mtoto wa kike waliyempa jina la Tiffany. Marla na Trump waliachana mwaka 1999.
Mwaka 2005 Trump alimuoa mwana mitindo mwingine Melania Knauss, huyu ni mzaliwa wa Slovenia. Mwaka 2006 akawa raia wa Marekani. Wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume, Barron.
Melania alipoulizwa katika mahojiano na CNN alisema: “hakuna nafasi ya kufikiri mambo madogo, hakuna nafasi ya matokeo madogo. Donald hufanya vitu vifanyike.
Hata hivyo, katika hali tofauti Melania aliwahi kumfananisha Trump na mtoto mdogo kwa kusema: “Mara nyingine husema nina wavulana wawili nyumbani. Ninaye mtoto wangu mdogo na ninaye mume wangu.”
Makala haya yameandaliwa na Hawra Shamte kwa msaada wa mtandao.
0 comments:
POST A COMMENT