Dar es Salaam. Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso) imevikumbusha vyuo vikuu nchini mambo wanayotakiwa kufanya ikiwamo kuelewa mikataba na nafasi ya wanafunzi katika masuala ya malipo ya ada vyuoni mwao.
Katika waraka wake uliotolewa kwa vyombo vya habari, Tahliso walilaani vikali kitendo cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kutangaza kuwazuia wanafunzi kufanya mahafali kwa kisingizio cha ada.
“Tahliso tumepokea malalamiko yenye kusikitisha kutoka kwa wanafunzi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) - MWANZA ambao wamehitimu katika mwaka wa masomo 2015/2016” amesema Stanslaus Kadugalize, Mwenyekiti wa Tahliso
Waraka huo umesema Mkataba wa malipo ya ada ni kati ya vyuo hivyo na HESLB na kuwa zipo taratibu zinazotumika kulipana ada hizo kati ya vyuo na Serikali kupitia HESLB;
“Wanafunzi hawajawahi kushiriki katika kupanga ada hizo, kufuatilia malipo ya ada hizo wala kutafuta fedha za kulipa ada hizo.” umesema waraka huo na kuongeza:
“Kwa sababu hizo, TAHLISO tunapinga vikali hatua hiyo iliyochukuliwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino na kuwataka wakuu wa taasisi za elimu ya juu nchini kutozuia wanafunzi kuhitimu masomo yao.”
Katika waraka huo Tahliso ilizitaka taasisi za elimu ya juu ambazo zinadai ada kutoka HESLB, kufuata utaratibu uliopo ambao umezoeleka wa kuidai HESLB na sio kuwaadhibu wanafunzi wahitimu.
UDAKU SPECIAL BLOG
0 comments:
POST A COMMENT