HOFU imetanda wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha baada ya tukio la kwanza la uchunaji ngozi kuripotiwa katika mji mdogo wa Karatu.
Binti mdogo mwenye umri wa miaka tisa, ameuawa mjini Karatu baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana wakati akielekea machungani na mifugo.
Mtoto huyo, Witness Andrew ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Darasa la Kwanza kwenye Shule ya Msingi ya Sumawe, alipatikana Jumatano usiku, akiwa tayari amekufa, baada ya kuripotiwa kupotea kwa zaidi ya saa 24 tangu alipoondoka nyumbani kwao akiwa anaswaga ng’ombe na mbuzi, Jumanne iliyopita.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwandani ambako mwili wa mtoto huyo ulipatikana, Alexander Lulu amesema maiti ta mtoto huyo ilikutwa ikiwa imetupwa shambani na baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa pamoja na ngozi iliyochunwa na kuondelewa kabisa.
Witness pia alikutwa bila mguu, mkono na sehemu zake za siri na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Tloma wanadai ni masuala ya ushirikina. Mtoto huyo ndiye wa kwanza kuchunwa ngozi katika eneo la Karatu na tayari hofu imeanza kutanda hapa, watu wakihofia kuwa wachuna ngozi watakuwa wamevamia wilaya hiyo.
Baba ya marehemu, Andrea Paulo na Mama Paulina Petro wanasema mtoto wao alipotea tangu Jumatatu wiki hii alipotoka na mifugo kwenda kuchunga kwenye uwanda wa Tloma, lakini hakurudi nyumbani, na kwamba mifugo aliyokuwa nayo ilirejea yenyewe.
“Tulimtafuta mtoto kila mahali, lakini bila mafanikio, hata tulipoikuta maiti yake eneo la Kiwandani, tulishangaa maana tulishapita kwenye mashamba hayo mapema, lakini hatukumuona,” walisema wazazi.
Wanakijiji wa Tloma wanaamini kuwa mtoto huyo alitekwa na kupelekwa eneo jingine ambako ndiko alichinjwa kabla ya wauaji wake kumrudisha na kumtupa Kiwandani
0 comments:
POST A COMMENT