Maoni ya baadhi ya wadau wa muziki kuwa kila wanapousikiliza ‘Salome’ wa Diamond na RayVanny wanapata picha ya matusi, yamekutana na majibu ya Boss huyo wa WCB.
Akifunguka jana kwenye kipindi cha Ngazi Kwa Ngazi kinachorushwa na EATV, Diamond alisema kuwa ‘Salome’ haina matusi bali imebeba lugha ya mahaba mazito.
“Ukiangalia wimbo wa Salome, hauna matusi, ila una maneno ya kimahaba,” alisema Mond.
“Unapozungumzia wimbo wa kimahaba, matusi yanatokea pale. Matusi yapo kwenye mahaba. Unapokuwa unaelezea masuala ya kimahaba utaonekana kama unatukana. Lakini sisi tumejitahidi kadri ya uwezo wetu mahaba yale kuyazungumza katika lugha ambayo ni ngumu sana mtu kuielewa,” alifafanua.
Kwa upande wake Ray Van, alisema kuwa pamoja na yote yanayosikika kwenye wimbo ule, wamejitahidi kutumia tafsida kuyaficha na ndio sababu wimbo ule unapendwa na watu wa rika zote na unaweza kusikilizwa hata katika jumuiya ya watu wanaoheshimiana.
Salome ni wimbo uliochukua mahadhi ya wimbo wa zamani wa Saida Kalori ‘Chambua Kama Karanga’ na umepata nafasi na mafanikio makubwa katika vituo vya runinga vya kimataifa na kuweka rekodi ya aina yake kwenye mtando wa YouTube.
Video ya Salome imeangaliwa zaidi ya mara milioni 13 na laki 7 kwenye YouTube.
0 comments:
POST A COMMENT