Kocha wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho amewajibu mashabiki wa Chelsea waliokuwa wakimuita ‘Yuda’ katika mechi ya Kombe la FA robo fainali dhidi ya Chelsea.
Sehemu moja ya mashabiki ilipiga kelele “F*** off Mourinho”, “Wewe si Special tena” na “ni Yuda” wakimaanisha msaliti katika ushindi wa Chelsea wa 1-0 katika uwanja wa Stamford Bridge.
Katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo Mourinho alijibu.
“Wanaweza kuniita chochote wapendacho. Hadi watakapopata meneja anayewashindia mataji manne ya Ligi ya Uingereza, Mimi ni nambari moja,” alisema Mourinho ambaye alitupiwa virago Chelsea msimu uliopita.
Katika vipindi viwili tofauti kama meneja wa Chelsea (2004-2007 na 2013-2015), Mourinho aliinoa Chelsea na kuipa mataji manne ya ligi, moja la FA na matatu ya Kombe la Ligi.
“Watakapopata mtu wa kuwapa mataji manne ya Ligi ya Uingereza, basi nitakuwa namba mbili. Lakini hadi sasa Yuda bado ni namba moja.”
0 comments:
POST A COMMENT