VINASABA vya faru John vinatarajiwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa vipimo vya vinasaba (DNA ) muda wowote kuanzia wiki hii baada kupatikana kwa mfadhili wa kulipia gharama za vipimo hivyo,
Faru John alizua gumzo nchini mwishoni mwa mwaka jana baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) na kuwatuhumu maofisa wa shirika hilo na wale wa Idara ya Wanyamapori kwa ‘kumuuza’ faru John kwa kampuni ya Grumeti kwa takriban shilingi milioni 200.
Kutokana na tuhuma hizo maofisa zaidi ya watano kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Idara ya Wanyapori na Tawiri walitiwa mbaroni kwa mahojiano na vyombo vya usalama. Hata hivyo, baada ya muda maofisa hao waliachiwa huru.
Kampuni hiyo ya Grumeti ambayo imewekeza katika shughuli za biashara ya hoteli, utalii na uhifadhi inamiliki hifadhi ndogo (sanctuary) ya Faru Weusi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aidha katika mfululizo wa matukio kuhusu sakata la faru huyo baadaye ilibainika alifariki dunia Agosti mwaka jana na waziri mkuu aliunda kamati maalumu kuchunguza kifo chake na pia kupimwa DNA.
Taarifa zilizofika kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimeeleza kuwa tayari nyaraka zote muhimu kuhusu kupelekwa kwa vipimo hivyo nchini humo zimekamilika.
Habari zaidi zinaeleza kuwa pamoja na kukabidhi nyaraka, maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii watakabidhi pia sampuli za vinasaba hivyo kwa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili visafirishwe kwenda Afrika Kusini.
Awali ilidaiwa kuwa kulikuwa na hali ya utata kuhusu nani hasa atalipa gharama za vipimo hivyo vya DNA baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kushindwa kupata fedha za kugharimia vipimo hivyo.
“Taarifa ni kwamba kuna mfadhili amepatikana (hakutaja jina) na kulipia gharama za vipimo vya DNA nchini Afrika Kusini katika maabara ya kupima vinasaba ambayo iko kitivo cha wanyama katika Chuo Kikuu cha Pretoria,” kilieleza chanzo chetu ndani ya Wizara hiyo.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa gharama za vipimo hivyo ni katika ya dola za Marekani 300,000 hadi 500,000 ambazo ni zinaweza kufikia kati ya shilingi za Tanzania milioni 700 hadi bilioni moja.
“Kwa kweli gharama za kufanya vipimo vya DNA ziko juu sana na serikali haikuwa na fedha zilizotengwa kwa kazi hiyo, amepatikana mfadhili ambaye atalipia gharama hizo hivyo muda wowote kuanzia sasa vipimo vitapelekwa Afrika Kusini baada ya kukamilika kwa nyaraka zote muhimu,” alieleza mmoja wa maofisa wa wizara hiyo aliyeomba asitajwe jina gazetini kwa kuwa si msemaji wa suala hilo.
Majibu ya vipimo hivyo ndiyo yanayotarajiwa kutengua kitendawili cha iwapo sampuli za vinasaba zilizochukuliwa kutoka katika mabaki ya mnyama huyo zinaoana na zile zilizoko kwenye pembe yake na kujua iwapo faru huyo alikufa kama watendaji wa Idara ya Wanyapori wanavyodai au la.
Juhudi za kumpata msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dorina Makaya hazikuweza kufanikiwa kutokana na simu yake kutokuwa hewani kwa muda mrefu lakini Afisa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Hamza Temba, alisema kwa kifupi kuwa suala hilo liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na pia Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Sidhani kama jambo hilo liko chini ya wizara kwa kifupi ninavyofahamu suala hilo liko chini ya ofisi ya waziri mkuu na pia mkemia mkuu wa serikali,” alisema ofisa huyo.
Maabara ya Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini ( Veterinary Genetics Laboratory – VGL)) kwa mujibu wa mtandao wa researhmatters.up.ac.za ilianzishwa mwaka 2009 baada ya kuwapo kwa wimbi kubwa la ujangili dhidi ya wanyama hao nchini humo.
Kwa mujibu wa mtandao huo wataalamu wa chuo hicho kitivo cha utafiti na tiba ya wanyama wakiongozwa na Dk. Cindy Harper walifikia uamuzi wa kuanzisha maabara hiyo kwa lengo la kukusanya sampuli za vinasaba kutoka kwa wanyama hao na kuhifadhi katika kanzidata (database) ya maabara ili zitumike kama sehemu ya ushahidi mahakamani katika kesi za ujangili wa faru.
Ugunduzi na uamuzi wa wataalamu hao ulitokana na kesi nyingi dhidi ya majangili kukwama na wengi kuachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi dhidi yao.
Kwa mujibu wa mtandao huo wataalamu hao wa chuo hicho hutumia sampuli za vinasaba na kuoanisha na alama za vidole vya majangili kisha kuwapa waendesha mashitaka ili kujenga ushahidi thabiti wa kuwatia hatiani washitakiwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa dunia ina faru wasiozidi 29,000 kati ya faru 500,000 waliokuwepo mwanzoni mwa karne ya 20 na Afrika Kusini ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao kwa sasa.
Kutokana na ujangili wa muda mrefu dhidi ya faru na mahitaji ya pembe zake katika nchi za kiarabu na zile za Asia ya Kusini ambazo wakati mwingine hutumika kama dawa za kiasili kumesababisha dunia kubakiza karibu asilimia moja tu ya faru.
Nchini Afrika Kusini pekee kati ya mwaka 2010-2015 zaidi ya faru 500 waliuawa na majangili na mwaka 2013 ulivunja rekodi kwa faru 1,008 kuuawa na majangili.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alishindwa kulitolea ufafanuzi suala hilo kwa maelezo kuwa alikuwa katika kikao cha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili.
0 comments:
POST A COMMENT