DAR ES SALAAM: Kama mbwai na iwe mbwai! Ndivyo wanavyosema baadhi ya wasichana wanaojihusisha na biashara haramu ya kujiuza (machangudoa) sehemu mbalimbali jijini Dar wakimaanisha liwalo na liwe baada ya kuamua kujilipua kwa Serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ na kurejea barabarani kuendelea kujiuza kama zamani.
Uchunguzi wa gazeti hili wikiendi iliyopita maeneo ya Kinondoni, Buguruni, Temeke, Manzese na mitaa mbalimbali ya Sinza jijini Dar ulibaini kuwa, machangudoa hao wamerejea upya barabarani baada ya kujificha kwa miezi kadhaa tangu walipopigwa marufuku kuifanya biashara hiyo.
Kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kiliwashuhudia wanawake hao na kufanya nao mahojiano juu ya kurejea barabarani ambapo walikuwa na maoni mbalimbali. Baadhi ya wanawake hao walifunguka kwa OFM kuwa, licha ya kupewa kashikashi na Jeshi la Polisi kwa kukamatwa na kupelekwa mahakamani, lakini hawawezi kuiacha ‘kazi’ hiyo kutokana na ugumu wa maisha.
Kwa mujibu wa baadhi ya wanawake walionaswa na OFM maeneo ya Sinza-Mori, Dar, walisema biashara hiyo ndiyo maisha yao lakini Magufuli amewanyoosha kwa sababu hata hivyo, dili hizo kwa sasa hazina pesa.
“Hatupendi kujiuza lakini tutafanyaje kwa sababu Magufuli ndiyo hivyo amebana, kama ni kutukamata acha tu tukamatwe hatuna jinsi. “Nani asiyependa kulala usiku na familia yake? Ukituona barabarani ujue hali ni mbaya, Magufuli alegeze kidogo basi,” alisema mmoja wa madadapoa hao.
“Kwa hali hii ya Magufuli, kama ni ambushi tupo tayari potelea mbali maana maisha yenyewe ndiyo hayahaya, kama vipi waturudishe vijijini maana hatuwezi kufa njaa, bila kujiuza tutakula nini? “Potelea mbali acha tu watukamate tukale ugali wa bure jela,” alisema mwingine kwa kujiamini.
Ijumaa lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Simon Sirro ili kumuuliza kama jeshi hilo limesitisha oparesheni za kuwaondoa machangudoa jijini Dar lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Gazeti hili linalishauri Jeshi la Polisi jijini Dar kurejesha zile oparesheni ambazo lilikuwa likizifanya kwani kwa namna moja ama nyingine kasi ya biashara hiyo ilipungua.
0 comments:
POST A COMMENT