WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka Japan na kusema kwamba kufanyika kwa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI) jijini Nairobi kumetoa fursa kwa Tanzania na nchi nyingine kukutana na wafanyabiashara wakubwa wenye nia ya kuwekeza barani humo.
Ametoa kauli hiyo Jumapili, Agosti 28, 2016 alipokutana faragha kwa nyakati tofauti na viongozi wa makampuni makubwa ya Japan ambao walikuwa wakihudhuria mkutano huo uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
Mkutano wa sita wa TICAD ambao umemalizika jana, ulilenga kuiwezesha Afrika katika sekta ya uchumi na uwekezaji. Ili kufikia lengo hilo, mkutano huo umewashirikisha wadau wa sekta binafsi zikiwemo kampuni binafsi zaidi ya 300 kutoka Japan.
Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Rais wa kampuni ya Sumitomo, Bw. Kuniharu Nakahura, alisema kampuni hiyo imeanza utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi II wa kuzalisha umeme wa MW240 kutoka gesi asilia (Gas Fired Combined Cycle Gas Power Plant). Mradi huo ulioanza kutekelezwa Machi 2016, unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Bw. Nakahura ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, alisema kampuni yao inajishughulisha zaidi na utengenezaji wa bidhaa za vyuma, kemikali, ujenzi wa miundominu, na usafirishaji.
Naye Makamu wa Rais wa kampuni ya Toyota Tshuso, Bw. Yasuhiko Yokoi alikutana na Waziri Mkuu na kumweleza jinsi kampuni hiyo kubwa duniani inavyoweza kushiriki na kuchangia maendeleo nchini Tanzania.
Alisema kampuni yao inajishugulisha zaidi na masuala ya miundombinu ikiwemo kuzalisha mitambo ya umeme na mitambo ya bandari. Pia inazalisha bidhaa za kilimo (matrekta, mashine za viwanda vya mbolea na nguo, ujenzi wa maghala ya nafaka), mitambo ya nguvu za umeme wa joto-ardhi na uzalishaji wa magari ya aina mbalimbali.
“Kwa mfano hapa Kenya, tumeweza kutengeneza mitambo midogo ya kisasa ambayo inazalisha mbolea tofauti kulingana na hali halisi ya udongo wa mahali husika. Huwezi kuzalisha mbolea ya aina moja na kuamua kuisambaza kwa nchini nzima. Tunapima udongo wa sehemu moja na kuzalisha mbolea inayofaa kwa udongo ule,” alisema.
Naye Rais wa kampuni ya Marubeni, Bw. Fumiya Kokubu alimweleza Waziri Mkuu kwamba maeneo ambayo wangependa kuwekeza ni kwenye viwanda vya nguo, mbolea, saruji, uzalishaji wa sukari, umeme wa gesi na hasa miradi ya LNG.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali iko tayari kushirikiana nao na akawashauri watume timu za maafisa wao ili wakutanishwe na wadau wa sekta husika.
Alisisitiza kuwa Tanzania hivi sasa imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kwa sababu hiyo inahitaji kuwa na nishati ya kutosha ili iweze kumudu kuendeleza sekta hiyo. “Serikali ya awamu ya tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda, tunahitaji kujenga viwanda vya kutosha ili tuweze kusindika mazao ya wakulima ambao wanafikia asilimia 80 ya Watanzania wote. Tunahitaji masoko ya uhakika kwajili ya mazao wanayozalisha,” alisema.
Akiwa kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu pia alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi, Bw. Filippo Grandi; Meya wa Jiji la Yokohama, Bibi Fumiko Hayashi; na Makamu wa Rais wa Kwanza wa Sudan, Jenerali Bakri Hassan Saleh.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alitembelea Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan (Africa-Japan Expo 2016) ambapo Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE) na wadau wengine kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) walishiriki.
Akiwa huko alitembelea pia mabanda ya Uganda, Rwanda, Sénégal, Kenya, Japan na UN Habitat. Pia alitembelea banda la wajasiriamali wa nguo kutoka Tanzania ambao walishiriki maonyesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 29, 2016.
0 comments:
POST A COMMENT