BUNGE linakusudia kuachana na mtindo wa kutambulisha wageni baada ya kipindi cha maswali na majibu kuanzia mkutano ujao wa Bunge isipokuwa kwa wageni wa kimataifa, lengo likiwa kuokoa muda wa shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria nchini.
Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa na Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyeliongoza Bunge hilo kwa mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa ya kuwa nje ya nchi alikokwenda kwa matibabu.
Alisema hayo baada ya kuongoza kipindi cha maswali na majibu na kusisitiza hayo yametokana na mapendekezo ya Kamati ya Uongozi ya Bunge.
“Kuanzia Bunge lijalo hatutambulisha wageni, labda wale wa kimataifa kwa sababu Watanzania tuko nao kila siku, si wageni katika nchi hii,” alisema Ndugai.
Tangazo hilo liliibua vicheko kwa wabunge, wanahabari na wageni waliokuwamo bungeni huku wengi wakionekana kukubaliana ikielezwa itasaidia kuokoa muda wa shughuli za Bunge.
Hata hivyo, alisema kama kuna wabunge wenye mawazo tofauti, bado wana fursa ya kuwasilisha ili yafanyiwe kazi kuona uzito wa hoja zitakazojengwa.
Kwa muda mrefu sasa, wageni mbalimbali wa wabunge wamekuwa wakifurika wakati wa vikao vya Bunge na wamekuwa wakitambulishwa bungeni, hali iliyotajwa kuchukua muda mwingi wa shughuli za Bunge.
0 comments:
POST A COMMENT