Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo atapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujitetea dhidi ya kesi ya madai ya Sh200 milioni iliyofunguliwa na waliokuwa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mgana Msindai na John Guninita.
Makonda anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Seneni Mponda atatoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Kwa upande wa Msindai na Guninita wao wanatetewa na mawakili kutoka kampuni ya Uwakili ya BM, Benjamin Mwakagamba na Ester Shedrack.
Katika kesi hiyo ya madai namba 68 ya mwaka 2015, Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Mwakagamba, walifungua kesi wakiiomba Mahakama hiyo ya Kisutu kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja wao kiasi cha Sh100 milioni.
Wanadai kiwango hicho cha fedha kutokana na maneno ya kuwadhalilisha yaliyotolewa na Makonda wakati akiwa Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), alipoitisha mkutano na waandishi wa habari.
Walalamikaji hao pamoja na hayo, wanaiomba Mahakama hiyo itoe zuio la kudumu kwa Makonda asizungumze tena maneno ya kashfa dhidi yao wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Pia, wanaomba Makonda kulipa riba na gharama za kesi.
Walidai kuwa Makonda wakati akiwa katibu uhamasishaji chipukizi wa CCM, katika mkutano wake alitoa maneno akidai kuwa Msindai na Guninita ni vibaraka wanaotumiwa kuharibu chama cha CCM kwa nguvu ya fedha.
Msindai na Guninita wanadai maneno hayo yaliyotolewa na Makonda yamewadhalilisha kwa jamii na kuwafanya waonekane kuwa ni watu wasiofaa kuwa viongozi.
Source: Mwananchi
0 comments:
POST A COMMENT