Rais John Magufuli amemteua Anne Kilango Malecela kuwa mbunge, huku akiwa mkuu wa mkoa pekee kwenye utawala wa awamu ya tano aliyedumu na wadhifa huo kwa muda mfupi wa siku 29.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Rais Ikulu, imeeleza kuwa Kilango ataapishwa kwa mujibu wa taratibu za Bunge.
Uteuzi huu unakuja siku chache kabla ya Rais Magufuli kumteua aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Kazi, Dk Abdallah Possi kuwa balozi. Tayari, Dk Possi amekabishi barua ya kujiuzulu ubunge.
Hata hivyo, Kilango anarudi katika ulingo wa siasa huku akiwa amepitia katika misukusuko kadhaa ikiwamo kupoteza kiti cha ubunge Same Mashariki, mkoani Kilimanjaro.
Kilango aliteuliwa Machi 13, 2016 na uteuzi wake kutenguliwa Aprili 11 mwaka huohuo, kutokana na kutoa taarifa kwamba Mkoa wa Shinyanga aliokuwa akiuongoza haukuwa na watumishi hewa.
Safari yake ya kisiasa
Mbunge huyo mteule alizaliwa Januari 9, 1956 Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. Mwaka 1979-1983 alikuwa mwalimu Sekondari ya Kisutu jijini Dar es Salaam; 1983-1991 alikuwa Mhasibu Msaidizi Shirika la Ndege Tanzania (ATC); na 1991-1993 alikuwa Mdhibiti wa Fedha Shirika la Ndege la Gulf.
Pia, mwaka 1993-1994 alikuwa Mhasibu Shirika la Ndege la KLM; 1994-2000 alikuwa akijishughulisha na ujasiriamali kwenye kampuni yake ijulikanayo kama Ninna Bridal Centre; 2000-2005 aliteuliwa ubunge na Rais Benjamin Mkapa; na 2005-2015 alikuwa mbunge wa kuchaguliwa Same Mashariki
0 comments:
POST A COMMENT