Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga amesema watu wawili wameripotiwa kupoteza maisha mkoani Mwanza kwa sababu ya kukosa dawa za kulevya mtaani kama walivyozoea.
Kamishna Sianga amesema taarifa hiyo ameipata kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, hali inayomaanisha mafanikio ya mapambano ya dawa hizo, ambapo kwa sasa usambaaji wake umepungua mtaani kwa kiasi kikubwa.
"Nimeongea na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ameniambia kwamba kuna watu wwili wamefariki sababu walikuwa drug addict na sasa dawa hizo hazipo mtaani" Amesema Sianga
Sianga amesema mara baada ya kupokea kijiti cha mapambano kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Mamlaka hiyo imeendelea na moto huo huo, na kwamba kwa hivi sasa timu yake hailali, ikiendelea na mapambano kila siku na kwamba hata leo, kuna mtuhumiwa mkubwa wa dawa za kulevya amekamatwa.
"Leo asubuhi tumemkamata mtuhumiwa mmoja mkubwa wa dawa kulevya, tupo naye tunaendelea kumuhoji, mengi yataibuka" amesema Kamishna Sianga
Kuhusu kuendelea kutumia mbinu iliyokuwa ikitumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam paul Makonda ya kutaja majina hadharani,, Kamishna Sianga amesema hatatumia njia hiyo kwa kuwa kutaja majina ya watu hadharani kunaweza kuiingiza serikali katika matatizo maana kuna watu wengine wanaweza kutoa majina ya watu kwa sababu ya chuki binafsi.
Amesema njia anayoitumia ni kuwakamata na kuwahoji kimyakimnya na wakishajiridhisha hatua nyingine za kisheria zinafuata.
Katika hatua nyingine, Sianga amesema Tanzania iko makini katika kuwashughulikia wahusika wakubwa wa dawa za kulevya duaniani tangu miaka mingi iliyopita, akitolea mfano mtuhumiwa mmoja wa kike ambaye ni gwiji katika biashara hiyo au 'King Pin', ambaye hivi sasa amefungwa katika magereza ya Tanzania tangu mwaka 2010
"Tulimkamata mmoja kati ya watu waliokuwa wametajwa kama king pin wa dawa hizo nchini Marekani, alikuwa ameshindikana, na huko Marekani alikuwa na kesi zaidi ya 40, lakini alikamatwa hapa na amefungwa tangu mwaka 2010, yuko gerezani nafikiri kama siyo Keko, ni Segerea". Amesema Sianga.
0 comments:
POST A COMMENT