DAR ES SALAAM: Mwanamuziki wa Injili Bongo, Flora Mbasha amezua gumzo la aina yake baada ya kudaiwa kuwatambulisha wachumba wawili tofauti katika Kanisa la Mchungaji Paul Bendera wa Kanisa la Ufunuo, Kimara- Bonyokwa.
Chanzo makini kilichopo kwenye kanisa hilo, kimeeleza kuwa, Flora ambaye sasa anatarajiwa kuolewa na jamaa anayefahamika kwa jina la Daud Kusekwa, awali alidaiwa kumtambulisha Peter Elias kama mchumba wake hivyo kuzua tafrani kwa waumini kuhoji kulikoni atangaze uchumba kwa watu tofauti ndani ya muda mfupi.
“Unajua tatizo linakuja ni kama Flora aliamua kubadili gia angani, awali alikuja kanisani kwetu na yule Peter ambaye pia mwanzoni watu walikuwa wakijua ni mlinzi wake, ghafla tukashangaa amemleta mtu mwingine na kusema ndiye atakayefunga naye ndoa.
“Huwezi amini hili suala litakuwa limempasua sana kichwa mchungaji. Watu hawawezi kukubali kwa lengo la kujenga nidhamu watataka kusimamia haki, kama ni yule wa awali ndiyo halali kutambulika kanisani au huyu mpya,” kilisema chanzo hicho ambacho kilijitambulisha kuwa kinasali kanisani hapo.
Mwanahabari wetu alimwendea hewani Mchungaji Bendera ambapo alikiri kuwafahamu Flora, Daud na Peter lakini akasema Peter alimtambulisha tu kama muumini hivyo hakuona sababu ya kumkataa Daud pindi alipotambulishwa na Flora kama mchumba wake wanayetarajia kuoana.
“Peter na Flora walikuja kama waumini. Lakini kama umesikia tofauti, nitawaita wote ili kuliweka sawa,” alisema mchungaji huyo.
Hata hivyo, chanzo kilichopo kanisani hapo kilizidi kumwaga ubuyu kuwa, mbali na uchumba huo kuzua tafrani kanisani hapo, kuna taarifa kuwa Flora anamtishia Peter kwamba amuache na asiingilie maisha yake na mpenzi wake wa sasa.
“Nasikia Flora anamtishia sana Peter hususan baada ya Peter kuwa anamtaka mwanaye ambaye amemnyang’anya. Sasa anamchimba kweli mkwara hadi jamaa imebidi atoe taarifa kituo cha polisi,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kunyaka ubuyu huo, mwanahabari wetu alimvutia waya Peter ambapo alipopatikana alikiri kupokea vitisho hivyo na kwamba ametoa taarifa katika Kituo Kidogo cha Polisi Tabata- Kisiwani.
“Ni kweli ananitishia lakini mimi siwezi kukubali mwanangu alelewe na mtu ambaye sina imani naye. Nitaenndelea kudai haki yangu,” alisema Peter huku akimtumia mwandishi wetu RB iliyosomeka, TBK/RB/37/2017 TAARIFA.
Alipoulizwa kama ameitwa na Mchungaji Bendera ili wakazungumzie suala lake akasema hajaitwa.
Kwa upande wake Flora, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, alisema hataki kabisa kuzungumzia habari za Peter.
Flora ambaye ameimba nyimbo nyingi nzuri za Injili ikiwemo Jipe Moyo, kabla ya kumuacha Peter na kuingia kwenye uchumba na Daud, aliolewa na Emmannuel Mbasha ambaye walitengana mwaka 2014.
0 comments:
POST A COMMENT