Askofu wa kanisa la ufufuo na uzima, Josephat Gwajima ameieleza mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuwa ofisa wa jeshi la polisi alitaka kumchoma sindano bila ridhaa yake wakati alipolazwa kwenye hospitali ya polisi Oysterbay.
Askofu Gwajima ameyasema hayo wakati akiongozwa na wakili wake Peter Kibatala alipokuwa akitoa utetezi katika kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha inayomkabili na wenzake watatu, mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Mbali ya Gwajima washtakiwa wengine ni mfanyabiashara anayedaiwa kuwa mlinzi wake, George Mzava, msaidizi wake, Yekonia Bihagaze na mchungaji Georgey Milulu ambao wanakabiliwa na kosa la kumiliki silaha isiyokuwa yao.
Katika utetezi wake, Gwajima alibainisha kuwa machi 27, 2015 anakumbuka alikuwa safarini kuelekea Arusha kwenye kikao cha maaskofu, ambapo aliondoka jijini Dar es Salaam, machi 26,2015.
Alieleza kuwa wakati alipokuwa njiani kuelekea Arusha aliona taarifa kwenye mtandao wa kijamii kuwa askofu Gwajima anatafutwa na jeshi la polisi.
Alieleza kuwa alishangaa kuiona taarifa hivyo, hivyo akafika hadi Arusha lakini alishindwa kushiriki katika mkutano huo badala yake alianza safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kwenye kituo kikuu cha polisi kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuripoti.
Gwajima alibainisha kuwa alifika jijini Dar es Salaam ambapo alikwenda kituoni hapo na kukutana na ofisa mpelelezi wa kanda hiyo na baada ya muda alianza kuhojiwa, wakati mazungumzo yakiendelea kulikuwa na mtu aliyekaa nyuma yake akisoma gazeti ambapo kulikuwa na kitu kikimpalia.
Ameeleza kuwa kutokana na hatua hiyo, alianza kupiga kelele kwamba kuna kitu kinamkera ndipo ghafla akajikuta amepoteza fahamu na hakujua nini kilichoendelea, alipopata fahamu alijikuta yupo hospitali ya polisi Oysterbay ambapo wakati akiwa kitandani alimuona mtu aliyevalia mavazi ya kipolisi ambaye alikuwa na nyota tatu.
Ambaye alitaka kumchoma sindano lakini alikataa na kuanza kubishana naye kwamba yeye ana daktari wake katika hospitali ya TMJ hivyo apelekwe huko na kwamba wakati akiendelea kubishana na askari huyo ghafla alijikuta kapoteza fahamu na alipozinduka alijikuta yupo hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Mkeha ameahirisha kesi hiyo hadi aprili 10 hadi 11, mwaka huu itaendelea kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo.
0 comments:
POST A COMMENT