Kamati iliyoundwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa Ofisi za Clouds Media Group, mchana wa leo imekabidhi ripoti hiyo kwa waziri huyo huku ikisoma mbele ya waandishi wa habari kile walichokipata katika uchunguzi waliofanya.
Mmoja wa wanakamati hao akisoma ripoti hiyo katika ukumbi wa Habari MAELEZO jijini Dar es Salaam alisema kuwa, kamati hiyo iliundwa ili kuchunguza sakata hilo na kuzisikiliza pande zote mbili kuhusu nini hasa kilitokea usiku wa Machi 17 katika ofisi za kituo hicho.
Kamati imeeleza kuwa baada ya kusikiliza upande wa Clouds Media Group kama alivyoeleza kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba walimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ili waweze pia kusikia yeye ana kipi cha kuzungumza.
Kamati ilimtafuta Makonda kwenye simu bila mafanikio na kuamua kwenda ofisini kwake ambapo walitakiwa kusubiri nje sababu alikuwa na ugeni wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene. Aidha baada ya kumaliza maongezi yao, wanakamati waliambiwa kuwa waelekee ukumbini kuonana na RC Makonda kwa ajili ya mazungumzo.
Aidha, walipofika ukumbini hawakumkuta na walibaini kuwa alitumia mlango wa nyuma kuondoka kwa madai anakwenda katika jengo la Machinga Complex na angerudi hivyo wamsubiri. Kamati ilimsubiri kwa muda mrefu lakini walipewa taarifa kuwa kiongozi huyo amepata dharura nyingine hivyo asingeweza kurejea kwa muda ofisini kwa ajili ya mazungumzo.
Kufikia hapo, kamati ilijiridhisha pasi na shaka kuwa RC Makonda amechagua kwa hiari yake kutozungumza nao kuhusu tukio analodaiwa kulitenda la kuvamia ofisi za Clouds.
Kuhusu kama ni kweli alivamia ofisi hizo, kamati imethibitisha kuwa RC Makonda alivamia ofisi hizo usiku akiwa pamoja na Askari wenye silaha ambapo alikwenda kwa gari aliyokuwa akiendesha yeye mwenyewe na pia wamesema sababu ya kuvamia ni kutaka kurushwa kwa kipindi chake alichorekodiwa mwanamke mmoja aliyekuwa akidai kuwa amezaa na Askofu Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Mbali na kuwa Makonda na Askari waliokuwa na silaha waliingia katika chumba cha kurushia matangazo kinyume na sheria, lakini kamati imefafanua kuwa aliwatishia watangazaji wale kuwa angewafunga jela miezi sita au kuwataja kwenye orodha ya watuhumiwa wa dawa za kuelvya kama wasingerusha kipindi hicho. Kutokana na vitisho vingi, watangazaji hao walishindwa kufunga kipindi cha SHILAWADU katika utaratibu unaotakiwa kwani ndio walikuwa wanamalizia.
Mbali na kuwatishia watangazaji hao, Makonda aliwatisha pia wafanyakazi wengine wa Clouds Media Group kuwa yote hayo yaliyotokea yabaki kuwa siri ndani ya ofisi hiyo, na kama mtu yeyote atathubutu kuyatoa nje ya ofisi, atamjua yeye ni nani.
Kamati imejiridhisha pasi na shaka kuwa Makonda alivunja sheria ya vyombo vya habari kwa kuingia katika kituo cha habari kinyume na sheria lakini pia kujivika kazi ya uhariri wa habari ambapo yeye si mtaalamu. Lakini pia, alivunja sheria kwa kushinikiza kipindi ambacho hakijahusisha pande mbili kurushwa hewani kitu ambacho ni kinyume na maadili ya utangazaji lakini pia sheria za vyombo vya habari.
Kuhusu RC kwenda Clouds, kamati imesema ni kweli huwa anakwenda mara kwa mara na hata siku moja kabla ya kufanya maadhimisho ya mwaka mmoja wa uongozi kama Mkuu wa Mkoa, alikuwa Clouds hadi saa tisa usiku akiandaa matangazo ya maadhimisho hayo. Lakini mara zote ambazo amekuwa akienda, hakuna hata siku moja alikuwa amefuatana na Askari au kuwa na silaha.
Watangazaji waliopiga kelele usiku ule imeelezwa kuwa si kwa sababu walipigwa mtama au kupigwa na vitako vya bunduki kama baadhi ya watu wanavyodai, lakini walikuwa wamejawa na hofu kufuatia uwepo wa askari katika chumba cha kurushiwa matangazo, imeeleza kamati hiyo.
Baada ya kamati kuyasema hayo yote kutokana na uchunguzi wao, walitoa mapendekezo ambayo wanaamini yanatakiwa kufanyiwa kazi haraka.
Miongoni mwa mapendelezo yaliyotolewa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda awaombe radhi Clouds Media Group kwa tukio lililotokea lakini pia awaombe radhi waandishi wa habari wote. Lakini pia imependekezwa Waziri husika ambaye ni Nape Moses Nnauye atoe taarifa kwa mamlaka husika ili Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda achukuliwe hatua.
Pendekezo jingine ni vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya Askari kuingia katika Ofisi za Clouds Media Group kinyume na sheria tena wakiwa na silaha za moto. Na pia Clouds wameshauriwa kutazama upya sera na sheria zao ili kuzuia watu wasiohusika kuingia bila idhini na kufanya kazi za uhariri wa vipindi au kazi nyingine bila kibali cha wamiliki.
Kuhusu Waziri Nape Nnauye, amesema kuwa ripoti aliyoipokea ataiwasilisha kwa mamlaka zilizo juu yake ambao wao ndio watakaoamua juu ya hatua za kuchukuliwa dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
0 comments:
POST A COMMENT