Mama mzazi wa msanii maarufu nchini, Wema Sepetu ametiwa mbaroni jijini hapa kwa madai ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mariam, ambaye ni mama mzazi wa mrembo huyo wa Tanzania 2006 alifikishwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay Jumamosi hi kwa madai ya kujipatia fedha hizo kutoka kwa mfanyabiashara, Alex Msama.
Habari kutoka katika kituo hicho zinadai kuwa Mariam alifunguliwa jalada la taarifa ya polisi Na. OB/RB/3358/2017 na alishikiwa kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa 12 jioni alipoandikisha maelezo na kudhaminiwa na watu wawili waliotajwa kwa majina ya Rose Moshi na Martha Mtiko.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hana taarifa na kuahidi kuzungumzia suala hilo leo.
Inadaiwa kuwa Mariam ambaye hivi karibuni yeye na binti yake huyo waliihama CCM na kujiunga na Chadema, alikubali kumuuzia Msama nyumba iliyopo katika Kiwanja 663 Block E, maeneo ya Sinza kwa Sh125 milioni.
“Nyumba hiyo ilikuwa inatakiwa kupigwa mnada na benki ya TIB kwa sababu mama Sepetu alikuwa amemdhamini mtu aliyekuwa amekopa katika benki hiyo, yule mtu aliposhindwa kulipa, watu wa benki wakataka kuipiga mnada,” chanzo chetu kutoka Polisi Osyterbay kilisema jana jioni.
Katika maelezo ambayo yapo kituoni hapo, inadaiwa kuwa Mariam alikubali kumuuzia nyumba Msama ili apate fedha za kuilipa TIB, lakini kwa wakati huo Msama hakuwa na kiasi hicho.
Inadaiwa kuwa wakati Msama akiendelea na mchakato wa kutafuta fedha ikiwa ni pamoja na kufuatilia mkopo kwenye benki nyingine ili ainunue nyumba hiyo, Mama Wema alikuwa akipewa fedha kidogokidogo ambazo zilifika Sh14 milioni.
Hata hivyo inadaiwa kuwa baada ya mama huyo kuona mchakato huo unachelewa aliuza nyumba kwa mtu mwingine bila kumtaarifu Msama, ambaye alijulishwa na dalali.
Jana, wakati wa mahojiano na polisi inadaiwa kuwa Mariam alikiri kupewa Sh8 milioni ambazo zipo kimaandishi na hatambui kuhusu fedha nyingine.
Msama alipopigiwa simu jana usiku alikiri kumshtaki mama huyo Polisi Oysterbay na kusisitiza kuwa anachotaka ni kulipwa haki yake.
“Ni kweli suala hili lipo Polisi kama mlivyosikia, sipendi kulizungumzia sana,” alisema Msama ambaye pia ni mwandaji wa matamasha ya injili.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alithibitisha kushtakiwa kwa kada huyo mpya wa chama chake na kusema aliandika maelezo kuhusu suala hilo na kuachiwa.
0 comments:
POST A COMMENT