Rais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe Spunda amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kujitokeza hadharani na kutoa ufafanuzi juu ya utata wa jina lake unaozidi kuvuma mitandaoni
Utata huo unadaiwa kutokana na mkuu huyo wa mkoa kutumia cheti cha mtu mwingine cha kidato cha nne kujiendeleza kielimu.
Rungwe ametoa ushauri huo kupitia kipindi cha maswali na majibu cha Kikaangoni , akimsisitiza Makonda kuweka ukweli mezani na kuacha kupiga chenga za mchangani kwa maana akiendelea kukaa kimya watu wanazidi kuamini uvumi huo.
"Namshauri Mkuu wa mkoa ambaye ni kama mwanangu, atoke azungumze ili kumaliza huu utata wa vyeti, asimsumbue Rais ana mambo mengi" Amesema Rungwe
Pia, amemtaka kuacha kulia madhabahuni, kwakuwa hilo halitamsaidia kwa kuwa kulia siyo jibu, na atambue kuwa ofisi hiyo aliyopo sasa siyo yake bali ni wananchi, hivyo kila alichokikuta atakiacha.
"Siku moja nafungua 'ipad' yangu namuona Mkuu wa Mkoa analia mbele ya kanisa halafu mchungaji anambembeleza kama mjukuu wangu, mimi namwambia kulia kwake hakusaidii kitu yeye anapaswa kusema ukweli tu kama hilo jina siyo la lake halisi ila ni la kisanii sisi tutamuelewa". Alisema Rungwe
Kwa upande mwingine, Rungwe ambaye ni wakili msomi, ametoa ushauri wa kisheria kwa watu wenye ushahidi na suala hilo kwenda mahakamani kwa kuwa sheria inaruhusu mashtaka binafsi, ingawa bado Jamhuri itahitajika zaidi kuisimamia kesi hiyo.
Aidha Rungwe aliendelea kufunguka kwa kumtaka Makonda kuacha kung'ang'ania nafasi ambazo anastahili katika nafasi hiyo huku akimpiga kijembe kuwa mwanaume hachagui kazi aende akabebe hata zege kama hana ujuzi wa kufanya.
Kwa upande mwingine Mzee Spunda amemuomba Rais Magufuli kuliingilia kati suala hilo kama alivyofanya kwa maafisa wengine wa serikali.
Rungwe alilazimika kutoa ushauri huo kutokana na swali aliloulizwa kuhusiana na maoni yake kuhusu vita dhidi ya dawa kulevya ambapo amesema kuwa anaunga mkono vita hiyo, isipokuwa njia iliyotumika ya kutaja majina ya watu hadharani bila uhakika, haikuwa nzuri.
0 comments:
POST A COMMENT