Hatimaye rapper Roma amesimulia mkasa wa kutekwa akiwa na wenzake watatu kuanzia Jumatano iliyopita hadi Ijumaa. Tumekuandikia kile alichosimulia.
Wakati naendelea na shughuli zangu, walifika watu ambao sikuweza kuwafahamu mbaya zaidi walikuwa na silaha za moto na amri yao ya kwanza ilikuwa ni ingia ndani ya gari. Baada ya kuingia tu ndani ya gari, nakumbuka wale watu walitufunga usoni na vitambaa na kutuamuru tuiname chini kwa order ya kwamba inama chini na usiinuke na wakiwa wameshika silaha za moto. Hofu yetu ikatufanya wote tuiname chini na gari ikaanza kuondoka maeneo ya studio na ikaelekea ambako sisi hatukupajua.
Tulipofika hiyo sehemu ambayo hatuijui tukiwa tumefungwa usoni, na walitufunga na pingu. Tukaenda sehemu ambayo hatuijui, kwa kuhisi tu hujui chochote na ndio sehemu ambayo tulikaa kwa siku zote tatu kwasababu ilikuwa ni Jumatano, Alhamis, tunakuja kupata sisi usalama ilikuwa ni Ijumaa usiku kuamkia Jumamosi. Kwahiyo siku zote watu kilichokuwa kinaendelea huko ambako tupo na hatupafahamu, kuna mahojiano yalikuwa yanaendelea baina yetu na wale watu, mahojiano yenyewe ndio hizo details ambazo nasema tumesharipoti katika vyombo vya dola wanaendelea na upelelezi, wakimaliza upelelezi, wao wenyewe wataongea watatoa taarifa.
Lakini mahojiano hayo yaliendana na vipigo ambavyo nimeonesha majereha. Kila mtu alipata majereha, kila mtu alipigwa, kwahiyo mahojiano yalikuwa yanaendelea na hizo torture mpaka siku ya Ijumaa usiku sababu hatukuwa tunaweza kugundua ni saa ngapi. Tulitolewa hapo tulipokuwepo na kuingizwa ndani ya gari na safari ilipoanza hapo tukiwa tumefungwa vilevile lakini safari hiyo tulifungwa na mdomo, tukafungwa na miguu tukiwa ndani ya gari tukaenda umbali ambao hatukuweza kujua ni wapi mpaka kufika eneo ambalo tukatupwa tukiwa katika hali hiyo wote wanne.
Ilikuwa ni usiku sanam hatukuweza kujua ni wapi lakini tulifikiri ni kwenye dimbwi tu la maji tumetupwa. Niliweza kujifungua mimi wa kwanza nikawafungua na wenzangu, hatukujua ni maeneo gani lakini yalikuwa maeneo ya baharini, tulikuwa na maumivu sana. Nilivyoweza kuwafungua wenzangu tukajikuta tuko salama, tukaanza kutembea kwa muda kiasi na baada ya muda tukakutana na kibao fulani kimeandikwa mahaba beach tukagundua kuwa pale ni maeneo ya Ununio. Tulitembea kwa umbali mrefu sana mpaka tulipoweza kupata msaada baada ya hapo tukaenda kuripoti maelezo yote katika kituo cha polisi.
ALIPOFIKA NYUMBANI
Tulipofika Mbezi mimi nagonga mlango, ndani hakuna mtu, nikazunguka mlango wa nyuma nikavunja mlango wa nyumbani kwangu. Kuingia ndani familia hakuna, hilo lilikuwa pigo jingine kwangu sababu sikujua familia yangu nayo imeenda wapi. hiyo ikawa hofu nyingine, kwahiyo tulichokifanya nikawaambia tubadilishe nguo nikachukua nguo nikawa wenzangu, tutokea katika zile nguo za matatizo. Nikawaambia kama familia haipo nadhani hapa si salama, ilikuwa inaelekea alfajiri saa kumi saa kumi na moja ikabidi tutoke tutafute bajaji tukiwa katika mavazi salama ikawa ni nafuu kwetu. Tulipotafuta bajaji tukaomba namba ya simu ya bajaji kumpigia mtu. Na mtu wa kwanza kumpigia ni bosi wetu J-Murder, hakutuamini kwamba ni sisi kwasababu ya kile alichokuwa anajua kinaendelea uraiani.
0 comments:
POST A COMMENT