NYOTA wa miondoko ya Hip Hop nchini, Roma Mkatoliki amejitokeza hadharani na kusema kuwa, kilichowakumba kwa kutekwa na watu wasiojulikana si kitendo cha kusaka kiki ama limetengenezwa kisiasa, bali ni la kweli na wameteswa.
Roma aliyetekwa pamoja na wenzake wawili katika studio za Tongwe Records, aliyasema hayo katika mkutano wake na wanahabari ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Msanii huyo aliyeonekana mnyonge alieleza kuwa tukio la kutekwa kwao sio kiki ama lililotengenezwa kwa kutumiwa kisiasa ila jambo lililotokea kweli na limewapa hofu kubwa kwa sababu hawakuwahi kuhisi litakuja kuwakumba.
"Kuna watu wanasema hii ni kiki, hawa watu wanafikiri tunafanya na wengine wameenda mbali sana kwamba tunatumika kisiasa. Wengine wanaenda mbali zaidi kusema kana kwamba wanajua zaidi," alisema Roma na kuongeza;
"Kuna watu wamesema tumepewa hela tufanye hivi, inaumiza sana kuna wasanii wengine wamesema kwamba tumepewa hela, si kweli. Sisi ni maskini na tunaishi maisha ya kawaida sana, hatuwezi kurisk (hatarisha) maisha yetu kwa sababu hiyo. Tunahisi itamtokea mwingine na tutakuwa katika nafasi mbaya sana."
Msanii huyo alifunguka namna walivyofuatwa na watu hao na kisha kuwapeleka kwenye gari kabla ya kuwafunga macho kwa vitambaa na kuanza kuwahoji, huku wakiwatesa mpaka walipotolewa kwenye gari na kutelekezwa wakiwa hoi.
"Ilikuwa ni usiku sana nilijitahidi kujifungua kitambaa na kamba. Nilifanikiwa na kuwafungua wenzangu tukaanza kutembea pasipo kujua Tunaenda wapi hadi tulipokikuta kibao kimeandikwa mahaba Beach ndipo tukagundua ni Ununio, baada ya hapo tukapata msaada wa polisi mpaka polisi Central," alisema.
Roma aliwashukuru wote wakiwamo wasanii kwa ushirikiano walioonyesha kiasi cha kuweka mbali itikadi zao kipindi chote alipokuwa haonekani, lakini akisisitiza kuwa hali ni mbaya na lazima serikali iwasaidie wasanii kuwa salama.
Alisema yeye na wenzake wamekuwa na hofu ya usalama wao, kwa namna hali ilivyowabadilikia wakati waliamini studio waliokuwa wakifanyia muziki ilikuwa salama kwao kabla ya kukumbwa na kisanga hicho, huku akieleza alivyoteswa kiasi fulana yake kuwa nyakanyaka kwa damu zilizomtoka, ingawa hakufafanua zaidi.
"Kama alifanyiwa daktari akaja akafanyiwa mwingine usishtuke kesho akafanyiwa daktari au yoyote. Wito wangu kuhusu hili kwa serikali tunaomba waziri atulinde bado hatuna Amani tangu juzi kuna picha inaingia bado tunahitaji ulinzi, watu wapaze sauti ili wasikie wengine kusaidia," alisema Roma Waziri Mwakyembe alisema ameshtushwa sana aliposikia taarifa hizi nilishtuka na kujiuliza kila chombo cha dola kimekiuka utaratibu wake wa kuwasiliana naye kwa tatizo lolote la wasanii.
"Ni lazima tujue nani amewafikisha wasanii wangu hapa, tunaomba ushirikiano wenu wote tumeshtushwa hili siyo jambo la kawaida kwa Watanzania. Siwezi kukubali tukachezea chezea watu hawa waliofanya kitendo hiki kwa sasa tumeunda vyombo vya upepelezi kupata majibu ya kina sana," alisema Waziri.
0 comments:
POST A COMMENT