Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia familia moja kukumbwa na mauzauza baada ya watoto wa mama aliyefahamika kwa jina la Hawa Hassan Ngonyani kupatwa na mabadiliko ya maumbile ambapo mmoja ameota matiti na mwingine kuanza kuotwa na uvimbe shingoni.
Hawa anaishi na wanaye watatu maeneo ya Kinzudi Kata ya Goba, jijini Dar ambapo waandishi wetu walifika na kujionea hali halisi ya watoto hao.
Mara baada ya waandishi wetu kufika katika nyumba hiyo, walipokelewa na Hawa aliyeonekana kukata tamaa ya maisha kutokana na jinsi anavyoishi kwa malumbano na mumewe anayedaiwa kuitelekeza familia yake.
Akizungumza na mwandishi wetu nyumbani hapo, Hawa alisema aliolewa ndoa ya mkeka miaka kadhaa iliyopita huku mwanaume akimzalisha ‘fastafasta’.
Alisema mwanaye mwenye umri wa miaka kumi na mbili anayesoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Kinzudi, alizaliwa mzima huku akiwa na chuchu mbili tu hadi mwaka jana mwanzoni ndipo alipokumbwa na balaa hilo la kuota chuchu zingine sehemu za juu ya titi za kawaida ambazo hadi sasa zinazidi kukua siku hadi siku.
Akizidi kufafanua, mama huyo alisema mara baada ya kuona hali hiyo, aliamua kumshirikisha baba watoto wake ambaye ni kama amehama kabisa nyumbani, lakini alikosa ushirikiano kwa mumewe huyo kwani hadi sasa mtoto hajapelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi, kwani zile chuchu zinazidi kukua pamoja na kumkosesha amani mtoto huyo anayejiandaa na mitihani ya kuhitimu darasa la saba.
Hawa alisema wakati akihangaika na mwanaye huyo wa kwanza namna ya kumpeleka hospitali bila msaada, mtoto wake mwingine ameanza kuota uvimbe shingoni ambao unahitaji jitihada za haraka kuutibu kabla haujawa mkubwa.
Na alipomueleza tena mumewe, pia hakumpa ushirikiano.
“Yaani alichonijibu ni kuwa yeye kwa sasa ana madeni mengi hivyo hana fedha, nifanye michakato mingine nikawatibu yeye hana hela kwa sasa,” alisema bi mkubwa huyo huku akibubujikwa na machozi.
Hata hivyo, dada huyo alisema mumewe ni mkorofi kwani pia amewahi kumpiga hadi kusaidiwa na majirani.
Mwanamke huyo alihitimisha kuomba msaada kwa taasisi na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu wamsaidie kumuachanisha na mwanaume huyo ambaye pia inadaiwa hutumia kilevi.
Hawa alisema anahofia usalama wake kutokana na kupigwa mara kwa mara na mbaya zaidi wakati anampiga huwa anamvua nguo zote na kumdhalilisha mbele ya watoto hivyo kukimbilia kwa majirani akiwa mtupu.
Aidha, pia mtoto huyo mwenye tatizo la kuota matiti ya ziada, alisema anaamini manyanyaso ya kutopewa huduma na mama yake kudhalilishwa vinatokana na mchepuko wa baba yake ambapo kuna siku alinasa mazungumzo live ya baba yake akiongea na mchepuko wake, lakini kikubwa kinachomuuma ni kulala na njaa au kunywa uji ambao hauna sukari.
Kufuatia tuhuma hizo, gazeti hili lilimsaka baba wa watoto hao aliyefahamika kwa jina la Abdul Liloka ili kuelezea kwa nini amekuwa akiinyima haki za msingi familia yake na hapa anaelezea tuhuma hizo:
“Ndugu mwandishi kwanza ni kweli mke wangu alinipatia taarifa za wanangu kuumwa lakini hali ya Magufuli sasa ni ngumu, mimi nilikuwa na madeni kibao ila kwa sasa nimemaliza nikipata hela nitampeleka hospitali huyu mdogo mwenye uvimbe.”
Kuhusu huyu mwingine mwenye matiti manne pia alisema: “Jamani hayo maziwa yaliyoota huo ndiyo utamaduni wa familia yetu, wapo dada zangu wengi wameota pia kwa hiyo hapo hamna tatizo tena bora hata yeye ni madogo yupo shangazi yake mmoja anayo makubwa balaa.”
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kuitesa familia yake kutokana na kuwa na mchepuko, Liloka alisema:
“Jamani mimi ni Muislam nina haki ya kuoa hata wanawake kumi si uwezo wangu, ni kweli nina mchumba mwingine nje hata huyo aliyewapa taarifa kwa maana ya mke wangu anamjua sana na kuhusu kumpiga ni kweli kuna siku nilimpiga kofi moja tu!”
0 comments:
POST A COMMENT