Tumaini jipya! Mtoto wa kiume wa mfungwa anayetumikia kifungo cha maisha jela, Nguza Viking ‘Babu Seya’, Mbangu Nguza ameibuka na kusema kuwa, mwaka 2017 ndiyo wa mwisho kwa baba yake na mdogo wake, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kuendelea kutumikia kifungo chao cha maisha jela.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Amani mwanzoni mwa wiki hii, Mbangu alisema kuwa, turufu ya mwisho ya hukumu ya ndugu hao ipo kwenye mikono ya Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCPHR) yenye makazi yake jijini Arusha ambayo kimsingi vikao vitatu vya awali vimeshakaa na kubaini kuwa, hukumu ya Babu Seya na Papii ilikuwa na kasoro.
“Unajua watu hawafahamu, kule ambako hukumu ya mzee na bwana mdogo (Papii), ilipelekwa kuna hatua. Kwanza kabisa, wale majaji wanatoka nchi mbalimbali, kwa hiyo siyo kwamba wanakwenda tu Arusha na kupitia hukumu, hapana.
“Kilichofanyika ni kwamba, kuna watu walikaa mara tatu kupitia hukumu ili wajiridhishe kama kuna makosa ambayo majaji wakikaa watayaona?
“Kwa hiyo vile vikao vimeshakaa mara tatu zote na kubaini kuwa, kweli hukumu ya baba na bwana mdogo ilikuwa ina kasoro.
“Sasa ndiyo majaji wameitwa ili kupitia na kutoa hukumu yao ya haki. Hii kazi ingekuwa imeshafanyika muda mrefu ila sasa, kilichotokea ni kwamba, kuanzia Novemba mwaka jana kama sikosei, watu wa mahakamani walikuwa likizo ndefu mpaka kwenye Februari mwaka huu, ndiyo wamerudi.
“Kingine kimechelewesha ni mwaka jana kustaafu kwa rais wa ile mahakama, Jaji Augustino Ramadhani (kutoka Tanzania), kukawa na kitambo cha kusubiri kumpata rais mpya, tayari yupo (Sylvain Ore kutoka Cote d’Ivoire).
“Kwa hiyo bwana, baada ya sasa, wakati wowote ule, majaji watatua Arusha na kukaa kupitia, naamini, tena narudia kusema, naamini, baba na bwana mdogo wangu mwaka huu watakuwa huru.
“Hili suala la wao kuwa huru liko pia kiroho, hata kama mahakama hiyo isingekaa, bado wale ndugu wangetoka tu, lazima. Kwani Mungu ninayemtegemea mimi ameshaniambia watatoka,” alisema Mbangu ambaye kwa sasa ni Mwinjilisti wa Neno la Mungu.
TUMEFIKAJE HAPA?
Nguza na wanawe watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa Kituo cha Polisi Magomeni, Dar, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16, mwaka 2003 wakituhumiwa kubaka na kunajisi watoto 10.
Baada ya kusikilizwa kesi hiyo Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanaye kwenda jela maisha kwenye Gereza la Ukonga, Dar es Salaam.
Januari 27, mwaka, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu.
Awali mwaka 2004, baada ya kukutwa na hatia katika kesi hiyo, Babu Seya, Papii Kocha na wakili wao, Mabere Nyaucho Marando walikata rufaa ya pili ambayo ilitupiliwa mbali.
Mwaka 2010 waliomba tena rufaa ambayo marejeo yake yalisikilizwa na kutolewa hukumu Februari, 2010. Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha, ikawaachia huru watoto wake, Mbangu na Francis Nguza.
0 comments:
POST A COMMENT