Miaka tisa baada ya kuvuliwa upadri wa Kanisa Katoliki, Privatus Kargendo jana alifunga ndoa na mchumba wake Rose Birusya. Ndoa hiyo ilifungwa katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam katika misa iliyoongozwa na Padri Stefano Kaombe.
Kabla ya kuvuliwa upadri, Karugendo alikuwa Padri wa Jimbo la Rulenge-Ngara kabla ya Papa Benedict XVI kumvua daraja hilo kwa madai ya kukiuka maadili ya kanisa katoliki.
Septemba 14, mwaka 2008 Karugendo alitangazwa kuwa ni muumini mlei asiye na daraja la upadri tena kupitia hati ya Papa yenye namba Protokali 4182/08.
Ingawa sababu za kuvuliwa kwake hazikuwekwa wazi kwa jamii zaidi ya kusema amekiuka kanuni za kanisa hilo, watu wengi walihusisha tukio hilo dhidi ya andiko lake kuhusu UKIMWI na matumizi ya mipira ya kiume (condoms).
Baada ya kuvuliwa cheo hicho, Karugendo sasa ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo gazeti la Mwananchi.
Waumini waliokuwamo katika misa ya ndoa hiyo, walimpongeza Karugendo na kusema kuwa uamuzi wake wa kufunga ndoa katika Kanisa Katoliki umeonyesha kuwa hana tatizo nalo licha ya kuvuliwa cheo hicho.
Mapadri wa Kanisa Katoliki hawaruhusi kuoa ikiaminika ili waweze kujikita zaidi katika kushughulikia masuala ya kanisa bila kuwa na kitu cha kuwaondoa humo ikiwa ni pamoja na familia.
0 comments:
POST A COMMENT