UTATA Waibuka Wakili Aliyefia Sebuleni Dar..Maiti Yake Yakutwa na Damu Kichwani. | KINGAZI BLOG

HABARI KARIBU YAKO ZAIDI.

Breaking News
Loading...

Saturday, 20 May 2017

UTATA Waibuka Wakili Aliyefia Sebuleni Dar..Maiti Yake Yakutwa na Damu Kichwani.


WAKILI wa kujitegemea, Noel Ndalu, amekutwa amefariki sebuleni nyumbani kwake Sinza jijini Dar es salaam, kifo ambacho kimeacha maswali kadhaa kutokana na mazingira yake.

Jana, Nipashe ilifika nyumbani kwa wakili huyo aliyekuwa akiishi Sinza kwa Remmy wilayani Kinondoni na kupata simulizi zenye kuibua maswali juu ya kifo hicho.

Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na sababu za kifo chake kilichoonekena kuwa cha ghafla, hasa kwa kutambua kuwa kazi zake huhusisha kesi zitokanazo na masuala mbalimbali ya migogoro ya kisheria wanayokumbana nayo wateja wake.

“Inasikitisha sana…kifo chake ni cha ghafla na kwakweli hatujui ni kitu gani kimemkuta…labda alikuwa akisumbuliwa na maradhi kama ya kifafa ambayo wakati mwingine huwafanya watu wanaoishi peke yao wapoteze maisha kwa namna hii. Hakuna anayejua kwakweli,” mmoja wa majirani aliiambia Nipashe kuhusiana na taarifa za kifo cha wakili huyo.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda, hakuweza kuzungumzia tukio hilo jana baada ya kueleza kuwa ametingwa na kikao, lakini baadhi ya majirani wameeleza kushangazwa na kile kilichomtokea mwenzao huyo.

Akizungumza na Nipashe, mama mwenye nyumba aliyokuwa amepanga wakili huyo, iliyopo katika Mtaa wa Mtendaji, Salama Shaaban (50), alisema Wakili Noel alikutwa amefariki sebuleni kwake juzi majira ya saa 4:00 asubuhi.

Alisema mara ya mwisho kuonana na mpangaji wake huyo ilikuwa ni Jumanne, saa 12:00 jioni wakati wakili huyo akimkabidhi stakabadhi ya uniti za umeme wa Luku aliokuwa amenunua.

“Jumanne alikuja hapa akaniambia mama nimekuletea umeme, nikamwambia ahsante mwanangu na alikuwa ni mzima wa afya...na tangu siku hiyo nikawa sijamuona kwa sababu anaishi upande wa pili wa nyumba yangu na ana geti lake,” alisema Salama.

Alieleza kuwa, hawakuwa na kawaida ya kuonana mara kwa mara na ndiyo sababu hakushtuka kutomuona kwa siku zote hizo.

“Hapa wako wapangaji wawili, marehemu na mwingine. Sasa jana asubuhi, nikiwa ndani kwangu, alikuja mpangaji mwenzake, akaniambia mama simu inaita muda mrefu ndani kwa Noel na hakuna anayepokea na yeye hajamuona akitoka,” alisema.

Alisema baada ya kupewa taarifa hizo, alitoka yeye na kijana wake kwenda hadi kwenye mlango mkubwa wa wakili Noel na kuanza kugonga. Walifanya hivyo kwa muda mrefu bila majibu na ndipo nao wakingiwa na wasiwasi.

“Chini ya mlango kuna uwazi hivyo mwanangu aliamua kuchungulia, akaniambia mama sioni kitu lakini nasikia harufu ya kitu kilichooza inatoka ndani,” alisema Salama.

Alisema mtoto wake huyo alichukua fimbo ndefu na kuipitisha chini ya mlango ambao upo karibu na dirisha kwa ajili ya kusukuma pazia ili waweze kuchungulia dirishani.

“Tulifanikiwa kusogeza pazia na tukachungulia ndani… tukamuona Noel akiwa amelala chali chini ya sakafu kuelekea mlango wa chumbani na kwenye paji lake la uso kulikuwa na damu zimechuruzikia kwa chini,” alisema.

Alisema baada ya kuona hali hiyo, waliamua kwenda kuwaita wajumbe wa mtaa wao ambao walifika na kushuhudia tukio lile kabla ya kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mabatini.

“Baadaye Polisi walikuja na gari. Waliamuru mlango uvunjwe, wakaingia ndani na kuuchunguza mwili. Wakakuta amechanika kwenye paji la uso wake,” alisimulia Mama Salama.

Alisema pia alikutwa amevaa kaptura na hawakukuta silaha ya aina yoyote. Baada ya hapo polisi waliuchukua mwili huo na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Mwananyala.

Akisimulia namna anavyomfahamu, Salama alisema wakili huyo binafsi ambaye alikuwa na ofisi yake Temeke jijini Dar es Salaam, ameishi kwenye nyumba yake kwa miaka mitatu.

Alisema awali alikuwa akiishi na mwanamke ambaye aliondoka miaka miwili iliyopita, na hivyo hadi umauti ukimkuta alikuwa akiishi peke yake.

“Mke wake aliondoka na mtoto wa miezi miwili. Kwa hiyo alikuwa akiishi peke yake,” alisema Salama.

Alisema baada ya kifo hicho, mjomba wake alifungasha mali za wakili huyo na kuondoka nazo na kwamba jana, waliuaga mwili wake katika Hospitali ya Mwananyamala na kusafirisha kwenda Dodoma kwa maziko.

“Baba yake anaishi Dodoma hivyo leo (jana) walienda Mwananyamala saa 4:00 kwa ajili ya kuuchukua mwili kuusafirisha,” alisema.

MAWAKILI WAMLILIA

Aidha, Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLC), kilitoa taarifa ya kifo cha aliyekuwa mwanachama wao mwenye namba ya usajili 4644, Noel Ndalu .

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa TLC kwa wanachama wake, ilieleza kuwa, mwanachama huyo alifariki Jumanne ya wiki hii, Mei 16 na kwamba aliagwa jana katika Kanisa la Kaloloni Chang’ombe na baadae kusafirishwa kuelekea mkoani Dodoma kwa maziko

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

    0 comments:

    POST A COMMENT

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us